Lugola: Tunamhitaji Lissu kusaidia upelelezi wa kesi yake

Muktasari:

Wakati mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu akiendelea na ziara zake nchini Marekani, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Kangi Lugola amemtaka kurejea nchini ili kusaidia upelelezi wa tukio lake la kushambulikwa kwa risasi


Arusha. Wakati mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu akiendelea na ziara zake nchini Marekani, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Kangi Lugola amemtaka kurejea nchini ili kusaidia upelelezi wa tukio lake la kushambulikwa kwa risasi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Februari 13, 2019 jijini Arusha, Lugola amesema Lissu ndio mwenye kesi hiyo, “Serikali inashindwa kuendelea na upelelezi wa tukio la kushambuliwa kwake kwa sababu haina mashahidi muhimu.”

Lissu alishambuliwa mchana wa Septemba 7, 2017 akiwa ndani ya gari, nje ya makazi yake Area D, mjini Dodoma wakati akitoka kuhudhuria mkutano wa Bunge.

Alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa matibabu ya awali na siku hiyohiyo alihamishiwa Hospitali ya Nairobi, Kenya.

Alipata matibabu katika hospitali hiyo hadi Januari 6, 2018 alipohamishiwa Ubelgiji.

Hivyo, tangu Septemba 7, 2017 hadi Desemba 31, 2018, mwanasheria huyo mkuu wa Chadema ametibiwa kwa kipindi cha siku 480 sawa na mwaka mmoja, miezi mitatu na siku 24. Siku hiyo ndio aliruhusiwa kutoka hospitali licha ya kuelezwa kuwa bado yupo katika matibabu. Katika gari hilo alikuwa pamoja na dereva wake Adam Bakari ambaye hakujeruhiwa na risasi na Lissu amekuwa akieleza jinsi alivyomuokoa.

“Hii ni kwa mara ya kwanza kutokea nchini mlalamikaji kutelekeza kesi. Kwanini  hataki kurudi kwenye kesi yake, aache kuwaeleza Wazungu  kwa sababu wanaopeleleza kesi ni sisi na sio wao,” amesema Lugola.

Waziri huyo ambaye pia ni mbunge wa Mwibara ameyataka mataifa ya kigeni kuja nchini kuwekeza na kuwapuuza watu wanaotoa taarifa potofu kuhusu amani na utulivu uliopo nchini.