Lugola aingilia kati migogoro ya ardhi inayowahusu polisi

Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Kangi Lugola akizungumza na wananchi wa kata ya Kimamba baada ya kupokea kero za wananchi hao za migogoro ya ardhi inayosababisha uvunjifu wa amani. Picha Hamida Shariff

Muktasari:

  • Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola leo Ijumaa amefanya ziara katika kata ya Kimamba mkoani Morogoro iliyokuwa na lengo la kusikiliza kero za wananchi wa kata hiyo

Morogoro. Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amesema wanasheria feki ndio wanaochangia migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro hivyo amewataka wananchi kutowatumia badala yake wafuate sheria.

Lugola ameyasema hayo leo Ijumaa Machi 15, 2019 kwenye kata ya Kimamba alipokwenda kusikiliza kero za wananchi wa kata hiyo ambapo alipokelewa kwa mabango yaliyokuwa na ujumbe mbalimbali.

Baadhi ya mabango hayo yameandikwa ujumbe 'polisi wa Dumila wanatumika kuwanyanyasa wananchi na polisi wa Chanzulu wanakamata watu na kuwaweka ndani wananchi wanaotafuta haki yao ya ardhi'.

Waziri Lugola amesema jeshi la polisi halihusiki na masuala ya ardhi isipokuwa limekuwa likichukua hatua pale migogoro hiyo inapoelekea kwenye uhalifu ama uvunjifu wa amani.

Amesema amefikia uamuzi wa kwenda kusikiliza kero za wananchi wa Kimamba ambazo nyingi zinatokana na migogoro ya ardhi ambapo mwisho imekuwa ikifikia kwenye uvunjifu wa amani.

Katika hatua nyingine, Waziri Lugola amemtaka kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Wilbrod Mutafungwa kuchunguza nyaraka zote za migogoro ya ardhi ili kujua kama ni halali ama zimeghushiwa.

Pia amemtaka kamanda huyo kuwachukulia hatua kali za kinidhamu askari wote wasiokuwa waadilifu watakaohusika kuwanyanyasa wananchi.

Hata hivyo, wananchi wameonekana kutokubaliana na uamuzi ya Waziri Lugola katika kutatua kero za polisi na wananchi zinazotokana na migogoro ya ardhi huku wananchi wakililalamikia jeshi la polisi kuwapendelea.

Mmoja wa wananchi hao Zainabu Nasibu amesema wapo baadhi ya wafugaji wamekuwa wakiwatumia polisi kuongeza nguvu ya kuchukua ardhi yao waliyokuwa wakilima kwa muda mrefu.