Lugola apokewa kwa mabango Kilosa

Saturday March 16 2019

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola 

By Hamida Shariff, Mwananchi [email protected]

Morogoro. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola jana alipokelewa kwa mabango yanayotuhumu polisi kuwanyanyasa, lakini akawatetea kuwa hawahusiki na masuala ya ardhi bali kuzuia migogoro kuvunja amani.

Pia alishauri wakazi wa Kata ya Kimamba, ambako alikwenda kusikiliza kero zao za ardhi, kutumia wanasheria wenye elimu wakati wa kufuatilia haki zao badala ya watu wa mitaani, ambao alisema ndio chanzo cha migogoro.

Moja ya mabango hayo liliandikwa “polisi wa Dumila wanatumika kuwanyanyasa wananchi” na jingine kuandikwa “polisi wa Chanzulu wanakamata watu na kuwaweka ndani wananchi wanaotafuta haki yao ya ardhi”.

Hata hivyo, waziri huyo alisema Jeshi la Polisi halihusiki na masuala ya ardhi, isipokuwa limekuwa likichukua hatua wakati migogoro hiyo inapoelekea kwenye uhalifu ama kuvunja amani.

Alisema amefikia uamuzi wa kusikiliza wananchi hao kwa kuwa kero zao nyingi zinatokana na migogoro ya ardhi inayotishia kuvunjika amani.

Waziri Lugola pia alimtaka Kamanda wa Polisi Mkoani Morogoro, Wilbrod Mutafungwa kuchunguza nyaraka zote za migogoro ya ardhi ili kujua kama ni halali ama zimeghushiwa.

Pia, alimtaka kamanda huyo kuwachukulia hatua kali za kinidhamu askari wote wasiokuwa waadilifu watakaohusika kuwanyanyasa wananchi.

“Wananchi mkiona hamuelewani kwenye masuala ya ardhi, tumieni vyombo vya sheria. Msijichukulie sheria mikononi wala msifanye vitendo vya uvunjifu wa amani, Rais Magufuli hapendi kuona migogoro ya ardhi,” alisema.

Advertisement