Lugola awekwa kati sakata la Lissu

Muktasari:

Wakati mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu akiendelea na ziara zake nchini Marekani, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Kangi Lugola amemtaka kurejea nchini ili kusaidia upelelezi wa tukio lake la kushambulikwa kwa risasi

Dar es Salaam. Chadema, wanasheria na wachambuzi wa siasa wamemshukia Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola baada ya kuhoji sababu za polisi kutomkamata Tundu Lissu na dereva wake kwa ajili ya mahojiano kuhusu shambulio la risasi la Septemba 7, 2017.

Lugola pia amehoji sababu za dereva huyo, Adam Bakari kutojeruhiwa na risasi takriban 38 zilizoelekezwa kwenye gari ambalo walikuwemo na Lissu na pia sababu za mbunge huyo wa Singida Mashariki kujeruhiwa upande wa kulia wa mguu wake badala ya upande wa kushoto zilikotokea risasi.

Lakini wachambuzi hao wamesema Lugola anapaswa kufahamu kuwa kurejea nchini au kumfuata Lissu aliko ni jukumu la polisi, huku mmoja wao akishauri kuwa kazi hiyo ifanywe na wachunguzi kutoka nje na si Jeshi la Polisi.

“Ina maana mpaka awepo (Lissu) ndio ichunguzwe?” alihoji Benson Kigaila, mkurugenzi wa operesheni na mafunzo wa Chadema.

“Anachotaka kusema Lugola ni kwamba hawatachunguza kupotea kwa Azory (Gwanda-mwandishi wa kujitegemea wa Mwananchi) na Ben Saanane (msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe) mpaka warudi.”

Alisema Serikali inapaswa kueleza uchunguzi ulipofikia na kushangaa sababu za Lissu kuitwa kusaidia uchunguzi wa kesi yake.

“Zipo kesi zilizowahi kufanyiwa uchunguzi japo wahusika walifariki. Wangekuwa na nia ya kuchunguza, wangeshajua aina ya bunduki iliyotumika, iliingizwa nchini lini na nani alikuwa anaimiliki kwa sababu kulikuwa na mabaki ya maganda ya risasi,” alisema.

‘Pande zote zinatuhumiana’

Mwanasheria maarufu nchini, Harold Sungusia alisema hakutakuwa na mshindi hadi kitakapopatikana chombo huru kuchunguza na kutoa taarifa ya tukio hilo.

“Hauwezi kuwa jaji kwenye kesi yako mwenyewe katika ile principle of natural justice (kanuni ya asili ya haki). Kwa kuwa huyo mmoja anaituhumu Serikali na Serikali inamtuhumu mhusika, hapo inatakiwa kipatikane chombo huru,” alisema Sungusia.

Alisema katika hilo Serikali ina doa na hivyo haiwezi kuunda tume yake kwa sababu tayari inatuhumiwa.

“Inaweza kuomba Jumuiya ya Madola, kwa mfano au (Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika) Sadc au ya Umoja wa Afrika kupitia mkataba wa Haki za Binadamu wa Afrika ili (ichunguze na) itoe ripoti,” alisema Sungusia.

Wakili, Fulgence Massawe alisema busara inahitajika ili kuondoa maswali, badala ya kuacha siasa iendelee kufunika sakata hilo.

“Kama tatizo ni imani kwa uchunguzi wa ndani, basi ikiwezekana Polisi iagize wachunguzi wa kutoka nje. Na si Lissu tu yako matukio mengi,” alisema Massawe.

Alisema suala la Lissu kupigwa risasi bado limegubikwa na kivuli kizito.

Lissu, ambaye yuko ziarani nchini Marekani alishambuliwa mchana akiwa ndani ya gari na dereva wake, nje ya makazi yake Area D jijini Dodoma wakati akitoka kuhudhuria mkutano wa Bunge.