Lulu ‘kafufuka’ mara tatu

Muktasari:

Ili uwe Lulu lazima uwe Elizabeth Michael.

Ni Jumamosi jioni. Moja kati ya hoteli zilizoibuka kama mvua za masika mitaa ya Sinza, nimetulia kaunta kwenye baa ya nje. Uso unatazama wapitao njiani kwa shida kutokana na mvua kuzalisha matope kila kona ya Jiji.

Katika meza moja jirani na kaunta warembo kadhaa wamekaa. Ni warembo mpaka wakaambukiza urembo wao kwenye pombe wanazokunywa, nazo zikawa na urembo fulani hivi amazing.

Mavazi kama wako kwenye movie. Wote macho kwenye simu zenye vioo vipana kama ‘kalukuleta’ za bodi ya mikopo. Wakawa kivutio kuliko nyama choma. Wanapiga soga ambazo zilipenya masikioni mwangu.

Wanamuongelea Lulu. Yes Elizabeth Michael. Baada ya habari kuwa kiumbe huyu katolewa gerezani na sasa atatumikia kifungo akiwa kitaa. Ni furaha kwa wengi siyo tu kwa mama na bwanaake.

Warembo wale walikuwa wanamuongelea Lulu huku wakitazama simu zao. Bila shaka mazungumzo yao yalianzia mitandaoni. Nyuso zao zilikuwa na shauku ya uwepo wa Lulu mtaani. Figo, mapafu na maini yao bila shaka yalichekelea taarifa hizo.

Sikushangaa wale warembo kumuongelea Lulu kwa namna ile. Namna iliyompendeza Mungu na kumkera shetani huko alipo. Njia alizopitia Lulu ni ngumu sana, kitu pekee cha kumsaidia yeye ni sisi kumuheshimu.

Kwa nini nisimuheshimu Lulu, ambaye Wema Sepetu alikuwa shabiki yake tangu akiwa kidato cha kwanza. Lakini mpaka leo Lulu kaendelea kuwa yule yule bila uwepo wa rangi ya pili (kujichubua) kwenye ngozi yake?

Kwanini nisimuhusudu Lulu ambaye kaanza kuigiza huku Rose Ndauka akiwa darasa la sita. Lakini yeye kaendelea kusimama kwenye sanaa ya uigizaji bila kujiingiza kwenye kazi nyingine yoyote.

Waigizaji wengi waliposhindwa kwenye sanaa wakajitumbukiza kwenye kazi zingine ili kuendesha maisha yao. Kwenye utangazaji na muziki. Yeye Lulu kabaki kwenye sanaa kama alama muhimu zaidi.

Kaanza kuwa staa Diamond Platinumz akiwa darasa la saba. Lulu ni mkongwe kwenye sanaa kuliko marehemu Kanumba. Wakati Lulu anaanza kuigiza Marehemu Kanumba alikuwa kidato cha tano hajui hata maana ya ‘scene’.

Lulu ni nguli kwenye sanaa kuliko Vincent Kigosi ‘Ray’. Wote hao wamemkuta Lulu akiwa juu kwenye kilele cha sanaa. Ameanza kuigiza Johari akiwa kwao huko Shinyanga, mpaka leo yupo juu kuliko Johari.

Mzee Chilo ni mkubwa kiumri lakini kwenye sanaa kamkuta Lulu. Ndivyo ilivyo kwa Mzee Korongo na Hashimu Kambi. Wote wamekuja baada yake, kwa nini ushindwe kutoa heshimu kwa Lulu? Kinachofurahisha ni kwamba kaendelea kuwa juu licha ya mitihani mingi aliyokutana nayo.

Mtihani wa kwanza Lulu alipitia kipindi kigumu zaidi cha makuzi. Kuvuka daraja la utoto kuja ukubwani, ni mtihani mkubwa zaidi duniani. Lulu kafanikiwa licha ya kuchafuka sana kwa skendo mbaya.

Na ieleweke kwamba ni binti ambaye kapitia na kushinda mtihani huu akiwa kakulia kwenye malezi ya mzazi mmoja wa kike. Kuwa pale alipo siyo jambo dogo na anastahili kuwa pale.

Wakati Christina Maningo ‘Sinta’, alimkuta Lulu kwenye sanaa, yeye skendo zikamuweka kando akashindwa kurudi kwenye kilele na kumuacha Lulu akiendelea kukimbiza kwenye sanaa.

Huu mtihani ulimshinda hata Nuru Nassoro ‘Nora’, skendo zilifunika kipaji chake. Wote wamehangaika kurudi bila mafanikio. Huku wakija wapya na kutoweka wakimuacha Lulu pale pale.

Ndiye msanii ambaye humuoni kwenye sinema kibwegebwege tu. Riyama anaweza kuwa bora ila kithamani Lulu ni mkubwa. Riyama anapatikana sana na kiwepesi. Lakini kumchezesha filamu yako Lulu ni gharama kuliko kugombea ubunge. Humuoni kwenye sinema za wasanii huku akiwa adimu hata kwenye sinema za baba yake mlezi Dk Cheni. Ni kwa sababu anajua thamani yake. Kajivisha thamani kubwa na imemuenea na ndiyo maana yuko pale.

Raha ya msanii ni kuijua sanaa yenyewe, ila raha zaidi ni kujua kuwa unajua. Hiki ndicho alichonacho Lulu, anajua kuwa anajua ndiyo maana habebeki kindezindezi kupelekwa ‘location’ kama mafungu ya nyanya.

Kuandaa stori ni kazi. Kuandika muswada ni jukumu zito.. Pia kupata washiriki kwenye nafasi husika siyo kazi ndogo. Ila kumpata Lulu ni kazi kubwa zaidi. Uliza watu wa filamu na wasanii.

Matukio yaliyomtokea kwa msanii mwingine angechezeshwa filamu nyingi sana. Lakini Lulu kwa kutambua thamani yake hajawahi kutumia maswahibu yake kama mtaji. Huyo ndiye Lulu anayekufanya ushangae kwa nini mzito sana tofauti na umri wake?

Mtihani wa pili mkubwa ni tukio la kifo cha Steven Kanumba. Akiwa rumande kwa miezi tisa, huku uraiani alikuwa adui namba moja kwa mashabiki wa Kanumba na sanaa. Alichukiwa kwa kiwango cha njaa na umasikini kama kielelezo cha msanii muovu.

Nani alitaka kumsikia Lulu? Msichana aliyewaondolea mpendwa wao? Steven Kanumba The Great kipenzi cha watu? Lulu alikuwa adui. Adui wa mashabiki wa filamu aliyefichwa kwenye kuta nne za gereza la Segerea.

Akapewa dhamana, na kuungana na ndugu na mashabiki uraiani. Tofauti na fikra za wengi. Lulu akatoa kazi iliyompa tuzo mpaka kwenye vibaraza vya mama zao kina Ramsey Noah huko Nigeria. Adui akageuka shujaa ghafla. Ogopa sana.

Hata kabla ya kifo cha Kanumba, aliwahi kutengwa na wasanii wa Bongo Movie. Dude akiwa msanii pekee aliyejitokeza na kumkemea kwa madai kuwa tabia zake zinatisha wazazi na kushindwa kuruhusu watoto wao kujiingiza kwenye filamu.

Lulu alipinda kweli kweli huku akijenga ushosti na pombe na kufunga ndoa na kumbi za starehe akiwa bado mdogo sana. Magazeti yalimuandika, watu walimsema. Lakini kwa umri wake hakutakiwa kutengwa na wasanii huku miongoni mwao wakimgeuza kama burudani ya nafsi zao licha ya kutenganishwa naye kiumri kwa miaka mingi.

Lakini alirudi kwenye mstari bila msaada wa wasanii wenzake. Huku wale wenye umri mkubwa zaidi yake wakitoweka kwenye ramani ya usanii. Na zaidi wakashindwa kurudi kwenye mstari walimuacha Lulu akielea kwenye boya la ustaa wenye ustaa.

Kina Shilole na mwenzake Snura walikimbia jukwaa la sanaa ya uigizaji. Madai yao filamu hazilipi na kujikita Kwenye muziki. Natasha na mwanaye Monalisa pamoja na Rose Ndauka, wanaishi kwa njia mbadala ya utangazaji wa radio.

Lulu hajawahi kuthubutu kufanya kazi nyingine nje ya uigizaji. Azam kumpa Ubalozi siyo bahati mbaya. Kama kweli filamu haziuzi, hebu weka mzigo wako kwa Lulu. Kisha mchezeshe filamu moja tu na uwapelekee

Wadosi kazi yenye sura ya Lulu. Utashangaa yale maandamano ya wasanii lengo lao lilikuwa nini?

Lulu ni pesa. Hata aliyempatia jina hilo la Lulu ni kama alioteshwa. Mazingira ya thamani yake ameyatengeneza. Ndiyo maana huwezi kumuona Lulu kwenye viwanja vya kipuuzi na makundi ya kibwege. Leo hii Lulu anatumikia kifungo chake akiwa nje ya kuta za magereza. Angalia kurasa za mitandao mbalimbali kila kitu kiko chini ya nyayo zake.

Watu wanampenda mtoto kwa sababu ya utoto wake. Kwa sababu ya sura ya utoto wake. Kwa sauti ya utoto wake. Kuingia katika utu uzima ni kazi nyingine ya kuwashawishi watu wakupende. Ngumu sana.

Maisha yake akiwa bado chini ya miaka 18 siyo haya aliyonayo hivi sasa, ni Lulu mwingine tofauti anayebeba dhamana ya Ubalozi wa kampuni kubwa kama Azam.

Wakati mwingine hawa madogo watazame kwa jicho la tatu. Endelea kukariri kuwa ukiwa mzuri na staa wa kike utapata maisha bora.

Mtazame huyu mtoto kwa jicho la tatu.

Alivuka makuzi ya utoto na skendo chafu za maisha yake. Akashinda mtihani wa kuonekana adui mkubwa baada ya kifo cha Kanumba. Na sasa ameendelea kuwa juu ya wasanii wengi waliomkuta kwenye sanaa.

Watoto waliozaliwa wakati anaanza sanaa ya uigizaji hivi sasa wana miaka 16 au 17. Wamezaliwa Lulu ni staa na bado ameendelea kuwa staa kwa kitu kile kile kilichompa ustaa tangu utotoni.

Ili uwe Lulu lazima uwe Elizabeth Michael.