Lulu Diva: Hakuna anayenibeba kwenye muziki

Saturday December 1 2018

 

Mwanamuziki wa Bongo Fleva Lulu Abbas amesema kinachomfanya asikauke katika majukwaa ni kujituma na si kitu kingine.

Akizungumzia tetesi za kwamba anapendelewa katika kushiriki tamasha la Fiesta lililomalizika wiki iliyopita amesema amechaguliwa kwa sababu yeye ni mkali wa jukwaa.

“Waandaaji wa tamasha hili wapo makini katika kuchagua wasanii watakaotumbuiza katika tamasha hilo, mmojawapo ikiwa ni pamoja na kujituma na kuwaridhisha mashabiki, jambo ambalo naamini nalifanya na ndio maana wamenichukua kwa mara nyingine,” amesema Lulu.

Mpaka sasa msanii huyu ambaye pia aliwahi kuwa Miss Kibaha mwaka 2013, ameshaachia nyimbo ambazo ni Usimwache, Amezoea, Utamu, Homa, Give it to Me, Alewa na Ona ambao alimshirikisha Rich Mavoko.

Kuhusu urafiki wake na Rich Mavoko na uhusika wake katika kuondoka WCB amesema hakumshauri chochote kwa kuwa ni mtu mzima.

Amesema hawezi kumshauri Rich katika jambo kama hilo kwani mbali ya kumtangulia katika muziki pia ana maamuzi na misimamo yake.

“Yaani mimi nimeanza muziki juzi, mwenzangu yupo kwenye game muda mrefu, nitamshauri nini kwa mfano, zaidi ya mimi kusubiri ushauri kutoka kwake,” amesema Lulu.


Advertisement