VIDEO: Lulu apania kumueleza Magufuli msongamano wa wafungwa

Tuesday February 12 2019

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Msanii wa filamu nchini, Lulu amesema akipata bahati ya kukutana na Rais John Magufuli atamuomba apunguze msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani.

Lulu aliyasema hayo jana alipofanya ziara katika ofisi za kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.

Hii ni mara ya kwanza kwa Lulu kufanya ziara Mwananchi ikiwa ni miezi mitatu tangu amalize kutumikia kifungo chake.

Msanii huyo ambaye jina lake halisi ni Elizabeth Michael amewahi kutesa na filamu mbalimbali ikiwemo ya Family Disaster, Foolish Age na A Woman of Principle.

Alihukumiwa kwenda jela miaka miwili Novemba 13,2017 baada ya kupatikana na hatia ya kumuua bila kukusudia msanii mwenzake, Steven Kanumba.

Katika mahojiano hayo pamoja na mambo mengine Lulu alipoulizwa ni jambo gani kubwa ambalo leo akikutana na Rais Magufuli litakuwa la kwanza kumwambia, alisisitiza kuwa ni hilo la msongamano wa wafungwa gerezani.

Msanii huyo alisema kwa kipindi alichokaa gerezani ameshuhudia uwepo wa msongamano kwa wafungwa na mahabusu jambo ambalo limekuwa ni kero. “Kiukweli watu gerezani wanasongamana mno, kuwa mfungwa haimaanishi upate shida ya kuishi kwa sababu wanastahili kupata haki zao kama binadamu wengine, kinachowatofautisha ni wao kukaa ndani na kupangiwa kila kitu cha kufanya,”alisema.

“Hivyo ombi langu kubwa kwa Rais aangalie hili suala la msongamano kwani limekuwa ni kero kiasi cha mahabusu na wafungwa kuona kama dunia imewatenga jambo ambalo si zuri, ”alisema.

Hata hivyo Lulu aliipongeza Mahakama kwa namna ambavyo imekuwa ikijitahidi kuendesha kesi kwa haraka tofauti na ilivyokuwa awali.

“Napenda kuona kasi hii ya uendeshaji kesi ikiongezeka maradufu ili anayetakiwa kufungwa ajijue mapema au anayetakiwa kuachiliwa aachiliwe akaendelee na kazi zake,” alisema Lulu.

Pia Lulu aliomba kama kuna uwezekano kubadilishwa kwa sheria kwa baadhi ya kesi zisizo na dhamana kwani mahabusu wa aina hiyo nao wanachangia kujaza magereza. Akilizungumzia hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya Parole Augustino Mrema alikiri kuwapo msongamano huo huku akieleza kuwa kumekuwa na juhudi zinazofanywa na Serikali kuondoa tatizo hilo.

Mrema alisema mojawapo ni kuendelea kumshauri Rais kutumia mamlaka aliyonayo kuachia wafungwa waliokidhi vigezo kila mwisho wa mwaka na kwenye sikukuu za kiserikali pamoja na kuwabadilishia aina ya vifungo wafungwa waliotumikia vifungo vyao zaidi ya robo tatu kwa kufanya kazi za kijamii.

Advertisement