Lusinde ataka polisi wawahoji Kinana, Nape sakata la sauti

Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde 

Muktasari:

Wakati sauti zinazosambaa mitandaoni zikidaiwa kuwa za Nape Nnauye na katibu mkuu wa zamani wa CCM, Abdulrahman Kinana zikizidi kuibua mjadala, mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde maarufu Kibajaj amemuomba Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kuwahoji wawili hao kwa madai kuwa wamemtukana Rais John Magufuli.


Dar es Salaam. Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde amemuomba Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kuagiza Jeshi la Polisi kumhoji Nape Nnauye na Abdulrahman Kinana kwa madai kuwa wamemtukana Rais John Magufuli.

Lusinde ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Julai 20, 2019 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam, wakati majibizano baina ya wanachama wa CCM yakizidi kupamba moto.

Lusinde, ambaye amepachikwa jina la “Kibajaj” alikuwa akizungumzia sauti zilizosambaa mitandaoni zikidaiwa kuwa ni za Nape, ambaye ni mbunge wa Mtama na Kinana, aliyekuwa katibu mkuu wa CCM, zikimtaja Rais Magufuli katika masuala mbalimbali.

Si Nape wala Kinana, ambaye hivi karibuni aliandika waraka kwa baraza la ushauri la viongozi wastaafu kulalamikia kuchfuliwa, aliyejitokeza kuzungumzia sauti hizo, wala hakuna waliothibitisha kuwa sauti hizo ni za makada hao, lakini Lusinde anataka wawili hao wahojiwe.

"Namshangaa Lugola,” alisema mbunge huyo.

“Watu wangapi hadi sasa wamefungwa kwa kumtukana Rais? Maneno waliyozungumza yamewatukana Watanzania. Sauti zinazosikika zina maneno ya fedheha, kitendo cha kusema Rais ni mshamba, amechanganyikiwa hakikubaliki.”

Hata Nape ameviachia vyombo vinavyohusika kushughulikia suala hilo.

Katika mahojiano na Mwananchi jana, Nape alisema hayupo tayari kuzungumzia sauti hizo zinazodaiwa kuwa ni za kwake kwa madai suala hilo lina ujinai na hivyo anaviachia vyombo vinavyohusika.

Pia alisema barua ya Kinana na katibu mkuu mwingine wa zamani wa chama hicho, Yusuf Makamba kulalamikia kuchafuliwa, akisema wanaodhani Rais John Magufuli hawezi kugombea urais mwakani wanapoteza muda wao.

Nape, ambaye amewahi kuwa katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, alisema anayedhani kuna uwezekano wa kumfanya Rais Magufuli asiwanie nafasi hiyo mwaka 2020 anajisumbua kwa kuwa utaratibu wa CCM Rais aliyepo madarakani, huwania tena nafasi hiyo awamu ya pili.