MKASA KUTOKA MOSHI: Mfungwa ajiua kwa kujichinja gerezani

Moshi. Agustino Moshi (70), mfungwa aliyekuwa anatumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa ubakaji, amejiua kwa kujikata mshipa wa fahamu kwa kutumia wembe akiwa ndani ya Gereza la Karanga mkoani Kilimanjaro.

Tukio hilo linadaiwa kutokea Jumatatu ya Juni 25 ndani ya gereza hilo na kushuhudiwa na mkuu wa gereza hilo, Kamishina Msaidizi wa Magereza (ACP), Leonard Moshy.

Habari ambazo zimethibitishwa pia na ACP Moshy zinasema mfungwa huyo mwenye namba 648/2015 alijikata na wembe kwenye mshipa wa fahamu shingoni mara tatu.

“Huyo mzee alitokea gereza la Maweni Tanga akaletwa kwa rufaa kwa ajili ya kutibiwa KCMC sasa siku hiyo walizozana na ACP Moshy na ndio akaamua kujiua mbele yake,” kilidokeza chanzo chetu cha habari.

Kwa mujibu wa mtoa habari huyo, siku hiyo saa 8 mchana, mkuu wa gereza alifika ndani ya gereza kwa lengo la kuwapangia wafungwa kazi ya kwenda shambani, lakini mzee huyo akadai anaumwa.

“Huyo mzee alimwambia bwana jela (ACP Moshy) kuwa ana ED (kibali cha daktari cha kupumzika) lakini bwana jela akakataa na ndipo huyo mzee akasema basi ngoja afe tu,” alidokeza mtoa taarifa.

“Hapohapo akatoa kiwembe akaanza kujikata shingoni kwenye mshipa wa fahamu. Yaani anaushika anajikata damu zinatiririka. Kama mara tatu. Lilikuwa ni tukio la ghafla ambalo kila mtu hakulitarajia”.

Baadaye askari magereza walifanikiwa kumkimbiza katika zahanati ya gereza kwa ajili ya matibabu ya kuokoa maisha yake, lakini hata hivyo kutokana na majeraha hayo alifariki dunia.

Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Gabriel Chisseo alilithibitishia Mwananchi jana juu ya kupokelewa kwa mwili huo na kwamba hadi jana, bado ulikuwa umehifadhiwa hospitalini hapo.

Uongozi wa gereza wafunguka

Mkuu wa Gereza la Karanga, ACP Moshy alithibitisha tukio hilo akisema ni la ajabu.

“Ni kweli alijikata mwenyewe akafa. Mimi sikuhadithiwa nililishuhudia mwenyewe. Sijawahi kuona mtu mwenye roho ngumu kama huyo. Yaani mtu anajikata damu zinatoka anajikata tu,” alisema.

“Yapo matukio yanayoweza kujitokeza gerezani sijawahi kuona tukio la aina hii wala hatujui kiwembe alikitoa wapi. Kuna mwingine aliwahi kujitumbukiza kwenye sufuria ya uji,” alisema.

Alipoulizwa iwapo kiini ni yeye kumlazimisha aende shamba, ACP Moshy alikanusha madai hayo na kusisitiza kuwa mfungwa huyo ni mmoja wa wafungwa ambao walikuwa hawataki kufanya kazi.

“Hawezi kulazimishwa. Mfungwa yeyote lazima afanye kazi. Hata mheshimiwa Rais (John Magufuli) amesema wafungwa wafanye kazi kwa hiyo ukija na kitambi utafanya kazi tu,” alieleza ACP Moshy.

ACP Moshy alifafanua kuwa siku hiyo alikuwa akikagua gereza na kupangia wafungwa kazi na alipomkuta mzee huyo alimuuliza mbona haendi shamba kulima kama alivyokuwa amepangiwa.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa gereza, mfungwa huyo alimwambia anaumwa lakini akamwambia asisahau kuwa anawajibika kwenda shamba kwa vile alishapona na ndipo ghafla akatoa wembe.

ACP Moshy alisema mfungwa huyo alianza kujikata shingoni kwa kutumia wembe huo huku akiendelea kufanya hivyo kwa kasi ya ajabu na walipomfikia tayari alikuwa amejijeruhi vibaya.

Mfungwa huyo alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa ubakaji mwaka 2015.