MO Dewji azua maswali mitandaoni, agusia kutekwa kwake

Muktasari:

  • Bilionea kijana nchini Tanzania na Africa, Mohammed Dewji ‘MO’ ameamua kutumia mitandao ya kijamii kueleza maswala mbalimbali huku akigusia swala la kutekwa kwake ambapo ameacha maswali mengi kwa wafuasi wake katika mitandao hiyo.

Dar es Salaam. Kama ni mfuatiliaji mzuri wa mitandao ya kijamii huwezi kuwa umepitwa na jumbe mbalimbali ambazo amekuwa akiziandika katika mitandao Bosi wa Klabu ya Simba ambaye ni Bilionea kijana Tanzania na Africa Mohammed Dewji maarufu MO.

Huenda watu wengi hawakuzoea kukutana na jumbe za bosi huyo katika mitandao mara kwa mara lakini kipindi hiki imekuwa tofauti ambapo siku za karibuni amekuwa akiandika jumbe mbalimbali nyingi zenye mafumbo ambazo zimekuwa zikiacha maswali kwa wafuasi wake mitandaoni.

Mo ni moja ya matajiri nchini ambapo siku za karibuni amepatwa na masahibu makubwa likiwemo lile la kutekwa na kupatikana baada ya siku kadhaa jambo ambalo limezidi kuchochea watu kufuatilia kila anachokiandika katika mitandao yake,

Kwa siku mbili  mfululizo tajiri huyo amekuwa akitumia mtandao wake wa Intsgram kutoa jumbe mbalimbali ambazo nyingine zimekuwa zikizua mijadala mitandaoni kila anapoziweka.

Jumamosi ya Juni 8, 2019 tajiri huyo aliibua utata katika mtandao wake wa Instagram baada ya kugusia tena swala lake la kutekwa huku akimshukuru mwenyezi Mungu ambapo katika ujumbe huo ukiambana na picha yake ulisomeka

“Unapopitia kipindi kigumu, unajuaje kama Mungu anakujaribu au anakuhukumu? Jibu ni linalokusogeza karibu na Mungu ni jaribu. Ambalo linakupeleka mbali na Mungu ni adhabu. Ukweli ni kwamba, kutekwa kumenisogeza karibu sana na Mungu” aliandika katika mtandao wa Instagram

Ujumbe huo ulizua minong’ono mingi mitandaoni huku wafuasi wake wakibishana kwa kasi wengine wakieleza huenda tajiri huyo kijana ana mengi ya kueleza kuhusu kutekwa kwake na huenda ameamua kukaa kimya.

meshackmichael14 alichangia ujumbe huo akisema, “Sawa Bos ila bado kutekwa kwako kumetuacha njia panda.” Huku chuwawilbald aliandika, “Mungu akubariki sana. Wasamehe na kuwaombea waliokuteka watambue dhambi zao na wafanye toba.”

sir_mnyamani aliandika, “Ni kweli kabisa matatizo humsogeza mja na muumba wake.” Huku shayovailethy, “Pole sana mzalendo wa taifa hili, Bible inaniambia kuwa ili dhahabu ing'ae lazima ipite kwenye moto, Mungu ana mpango na wewe usiache wala kuchoka kumtegemea.”

Wakati watu wakiendelea kuutafakari ujumbe huo wa Jumamosi siku iliyofuata yaani jana Jumapili, aliweka ujumbe mwingine ambao nao uliwafanya wafuasi wake kuendelea kushambulia kurasa yake ya Instagram wakiamini huenda kuna kitu bosi huyo anacho kichwani na ameamua kukisema kwa njia ya mafumbo mitandaoni.

Katika ujumbe huo wa Jumapili aliandika “Ni ngumu sana kutengeneza milioni kuliko bilioni. Ni rahisi kuzidisha pesa kuliko kupata pesa bila kuwa na kitu” aliandika na kisha kuutafasiri kwa Lugha ya kiingereza “It‘s more difficult to make a million than a billion. It’s easier to multiply money than to make money out of nothing.”

norbertmartin5 amesema, “Kweli kabisa boss wetu lakini vipi kuhusu usajili katika kikosi cha simba.” Naye mwasiree amesema, “Nimekuelewaaa maneno yako Mungu akulinde.”

Tukio la kutekwa na kupatikana kwa tajiri huyo liliacha maswali mengi nchini hasa baada ya ukimya wake baada ya kupatikana lakini sasa ameamua kutumia baadhi ya tungo tata mitandaoni kueleza kuhusu swala hili

Soma zaidi: