MSD yawataka wafanyabiashara kujenga viwanda vya dawa

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu

Muktasari:

  • Bohari ya Dawa (MSD) imewahamasisha wafanyabiashara wa ndani kujenga viwanda ili kuzalisha dawa zenye ubora kwa wingi tunapoelekea uchumi wa kati wa viwanda, kwani uhakika wa soko upo.

Dar es Salaam. Bohari ya Dawa (MSD) imetangaza fursa kwa wafanyabiashara wanaotaka kuanzisha viwanda vya dawa nchini kujitokeza kwa wingi ili kuweza kuzihudumia nchi 16 ambazo ni wanachama wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

MSD imesema umakini wa Serikali uliifanya nchi iteuliwe kuwa mnunuzi mkuu wa dawa, vifaatiba na vitendanishi kwa ajili ya SADC.

Akizungumza jana usiku Januari 19, 2019 katika mahojiano maalum kupitia kipindi cha Mizani kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema kutokana na mifumo iliyopo sasa ilikuwa rahisi MSD kushinda zabuni hiyo.

Alisema kutokana na heshima ambayo nchi imepewa pia hiyo ni nafasi nzuri kwa wafanyabiashara wa ndani kujenga viwanda ili kuzalisha dawa zenye ubora kwa wingi tunapoelekea uchumi wa kati wa viwanda.

“Umakini wa Serikali na mifumo mizuri hasa ya ununuzi na ugavi tuliyonayo kwa sasa, uliifanya MSD ishinde zabuni kwa kuwa pia tulishaingia katika ununuzi wa bidhaa zetu moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji hii ilikuwa ni sifa moja,” alisema Bwanakunu.

Alisema namna watakavyoweza kuzihudumia nchi hizo kwa kutumia mfumo maalum wa manunuzi kupitia mtandao.

“Tutasimamia mfumo wa manunuzi kwa njia ya mtandao kwa nchi zote wanachama, kazi yetu kubwa itakuwa ni kupokea mahitaji ya manunuzi, kununua kupitia wazalishaji moja kwa moja na dawa hizo zitatumwa katika nchi husika kulingana na oda zao,” alisema.

Alisema kazi ya MSD itakuwa ni kusimamia takwimu na taarifa zitakavyohitajika, kusimamia kanzi data, kutengeneza na kusimamia ununuzi wa dawa, vifaatiba na vitendanishi kwa ajili ya nchi hizo na kusimamia mnyororo wa ugavi.

Novemba 2017, Serikali kupitia MSD ilitangazwa rasmi kuteuliwa kuwa mnunuzi mkuu wa dawa, vifaatiba na vitendanishi vya maabara kwa nchi hizo, uteuzi uliofanyika katika mkutano wa SADC na mawaziri wa afya wa nchi wanachama na Oktoba 8 mwaka 2018 MSD na sekretarieti ya SADC walisaini makubaliano ya mkataba huo.