Ma DED waonywa kutumia fedha za mifuko ya jimbo

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, Mwita Waitara akijibu maswali ya wabunge wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Fedha za mifuko ya jimbo hutolewa kwa kila jimbo kwa lengo la kuchochea maendeleo jimboni na mwenyekiti wa fedha hizo ni mbunge. Serikali ya Tanzania imetoa onyo kwa wakurugenzi kutoingilia matumizi ya fedha hizo.

Dodoma.  Serikali ya Tanzania imetoa onyo kwa wakurugenzi wa halmashauri nchini kutozitumia fedha za mifuko ya jimbo bila idhini ya mbunge kwani hawana uamuzi na fedha hizo.

Onyo hilo limetolewa leo Jumatatu Mei 13, 2019 na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Konde (CUF), Khatibu Said Haji.

Katika swali lake, Haji ametaka kujua iwapo kuna baadhi ya wakurugenzi hufanya matumizi ya fedha za mfuko wa jimbo bila kuwashirikisha wabunge hususan Zanzibar, Je, katika hili suala la kusimamia fedha hizi ni la mbunge au wakurugenzi.

Akijibu swali hilo, Mwita amesema mwenyekiti wa fedha za mfuko wa jimbo ni mbunge na wajumbe wanajulikana kwa mujibu wa sheria, kanuni na mkurugenzi anapaswa kuheshimu uamuzi wa kamati hiyo ambayo mbunge ndiyo mwenyekiti wake.

Mwita amesema kama mbunge ataridhia fedha hizi kutumika sehemu fulani mkurugenzi hawezi kuzuia, kama mbunge atakwenda eneo A au B na kusikiliza kero za wananchi na kuahidi kutoa Sh500,000 mkurugenzi hawezi kubadilisha.

“Wale wakurugenzi wenye tabia ya kutumia fedha za mfuko wa jimbo tunaomba majina yao na ndio maana fedha zikishapitishwa na kamati ya mfuko wa jimbo mkurugenzi hawezi kubadilisha,” amesema Mwita huku wabunge wakishangilia.

Baada ya majibu ya Mwita, Spika Job Ndugai akatumia fursa hiyo kuwakumbusha wabunge kuzingatia miongozo ya kamati ili isije kufikiriwa ni mbunge pekee pasina kamati ya fedha hiyo kuhusishwa.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisimama kuzungumzia suala hilo akisema, “Kwa makofi haya ya wabunge kutokana na majibu ya Serikali inaonyesha yako matatizo katika uendeshaji wa fedha hizi.”

“Usimamizi wa mfuko wa jimbo lengo lake ni kuhakikisha wabunge wanachochea maendeleo katika maeneo yao hivyo tunaomba Serikali mtuachie ili tukashauriane na waziri mwenye dhamana ikiwezekana Serikali itoe tena waraka ili kila halmashauri iweze kusimamia utekelezaji wa mfuko huo na tuwaombe wabunge ambao ni wenyeviti wa fedha hizo matumizi yazingatie sheria,” amesema Waziri Mhagama.

Spika Ndugai akahitimisha kwa kusema, “Hilo litasaidia sana mkitoa waraka.”