Ma RC-DC wanaoweka watu mahabusu bila sababu kushtakiwa

Tuesday April 16 2019

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika akijibu hoja za wabunge waliochangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi 

By Fidelis Butahe, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Kapteni mstaafu George Mkuchika, amesema wakuu wa mikoa na wilaya watakaowaweka watu ndani kinyume cha sheria, watashtakiwa wao binafsi, hawatatetewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Namshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa waraka kwa wote waliopewa mamlaka ya kuweka mtu ndani na miye kanipa nakala, ikieleza mazingira ya mtu kuwekwa ndani,” alisema Mkuchika jana bungeni, Dodoma.

Akijibu hoja za wabunge walizozitoa katika mjadala wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2019/2020 iliyopitishwa jana jioni, Mkuchika alifafanua, “Moja awe ametenda kosa la jinai, na (mkuu wa wilaya, mkoa) uweke kwa maandishi kwa nini umemuweka ndani. Utawala bora unasema kesi ikiwa mahakamani hakuna mkuu wa wilaya, mkoa au waziri anayeweza kuisikiliza.”

“Uamuzi wa mahakama ya chini ya unaweza kutenguliwa na mahakama ya juu wengine wamejiingiza katika matatizo kwa mambo ambayo tayari yametolewa hukumu mahakamani.”

Alisema wakuu wa wilaya na mikoa wanapotumia mamlaka yao kumuweka mtu mahabusu saa 24 na 48 wazingatie sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997.

“Sheria hii inawapa mamlaka kuwaweka ndani watu pale inapothibitika anahatarisha amani. Nawaomba wabunge tusisitize sheria na nawaomba na huko walipo (wakuu wa wilaya na mikoa) wanisikilize,” alisema.

Advertisement

“Mtu anawekwa ndani kama amehatarisha amani, si watu wanadaiana madeni hawataki kulipa unawapeleka kwa mkuu wa mkoa, hawa wanadaiana si kuhatarisha amani.”

Alisema viongozi hao wakitekeleza hatua kinyume na utaratibu wanaweza kuchukuliwa hatua ikiwamo kushtakiwa binafsi.

“Tumekemea sana hili jambo, sasa hivi mwanasheria wa serikali hatomtetea mtu aliyevunja sheria makusudi kwa kumuweka mtu ndani bila sababu. Utapelekwa mahakamani na huyo uliyemuweka ndani na mwanasheria hatokuja kukutetea,” alisisitiza.

Haki kwa wananchi

Alisema kuna mifumo imewekwa kuhakikisha vyombo vya Dola vinatenda haki na kunapokuwa na ukiukwaji wa sheria hatua huchukuliwa. “Matukio ambayo yamebainishwa kwa mwananchi Musa Adam Said kubambikiwa kesi ya mauaji, ni upungufu wa watendaji wachache tulionao. Rais (John Magufuli) ameagiza waliohusika na tukio hilo wachukuliwe hatua,” alisema Mkuchika.

Uwazi

Kuhusu Tanzania kujitoa katika mpango wa uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa uwazi, Mkuchika alisema Tanzania imejitoa katika mpango huo, lakini ipo katika Mpango wa Waafrika Kujitathmini Uendeshaji wa Serikali kwa Uwazi, “niwatoe hofu, Tanzania bado tunaendesha Serikali kwa uwazi na ukweli. Tungekuwa tunaendesha Serikali kimya tusingeleta ripoti za CAG bungeni.”

Viashiria vya ubaguzi

“Watu wa upinzani, CCM na wasio na chama wanataka amani. Tushirikiane wote kukemea inapotokea dalili kama hizo. Rai yangu tushirikiane kukemea kwa nafasi yake,” alisema Mkuchika.

Takukuru

Kuhusu kutaka Takukuru kuwa huru na kufanya kazi bila kuingiliwa na mamlaka yoyote Mkuchika alisema, “Takukuru kazi yake ni kupeleleza na kupeleka mashauri mahakamani na mengine kupitia kwa DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka).” “Lakini anayeamua mtuhumiwa ana kosa au la ni hakimu au Jaji, nafasi ya Takukuru kumtia mtu hatiani bila ushahidi haipo.”

Kuhusu watendaji wa Takukuru kutoteuliwa na Rais, alisema, “Takukuru wanafanya kazi kama jeshi na Rais wa nchi cheo chake kingine ni amiri jeshi mkuu. Watendaji wote wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa sheria tulizojiwekea wanateuliwa na Rais.”

Akizungumzia Takukuru kushtaki wafanyabiashara kwa kuwabadilishia makosa yanayohusu kiasi kidogo cha fedha na kuyafanya uhujumu uchumi alisema, “kwa mujibu wa aya ya 21 jedwali la kwanza la sheria ya uhujumu uchumi ya mwaka 1984 makosa yote yanayoainishwa kwenye sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba hiyo isipokuwa tu kwa kifungu cha 15, ni makosa ya uhujumu uchumi.”

“Kuhusu watuhumiwa kushtakiwa kwa makosa ya utakatishaji fedha ni vyema ikafahamia kuwa kifungu cha 3 cha sheria inayohusu kutakatisha fedha namba 12/2006, kosa la rushwa ni moja wapo ya yanayosababisha mtumishi kushtakiwa kwa utakatishaji fedha. Wanashtakiwa kwa sheria tuliyonayo.”

Advertisement