Maalim Seif: Haki ya Wazanzibari haizami

Mwanachama wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza wakati wa mahojiano na waandishi wa magazeti ya Mwananchi Communications Limited, nyumbani kwake jijini Dar es Salaam. Na Mpigapicha Wetu

Muktasari:

Hata hivyo, kauli hiyo iliwahi kujibiwa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein akiwataka Wazanzibari kuacha kusikiliza “maneno ya propaganda kutoka kwa wapinzani” kwa kuwa katu hakuna rais mwingine atakayeongoza Zanzibar wakati yeye yupo madarakani.

Kwa nyakati tofauti tangu kumalizika kwa uchaguzi wa Rais Zanzibar mwaka 2015 uliofutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na ule wa marudio kususiwa na CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amekuwa akitoa ahadi maalumu kwa wafuasi wake akitaka “wawe na subira mambo mazuri yanakuja”.

Maalim alisusia uchaguzi wa marudio ulioitishwa na mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha Machi 20, 2016 akidai matokeo halali ni ya ule wa Oktoba 25 ambao anaamini alikuwa ameshinda.

Hata hivyo, baada ya kufutwa kwa madai ya kuwepo mapungufu, mshindani wake, Dk Ali Mohammed Shein (CCM) alishinda nafasi hiyo katika uchaguzi huo wa marudio.

Baada ya hali hihyo, mara kwa mara Seif amekuwa akiwataka wafuasi hao “kutokata tamaa, wawe na umoja na utulivu na kwamba haki yao ya mwaka 2015 ipo na ingepatikana hivi karibuni.”

Seif amekuwa akitoa kauli hiyo katika maeneo tofauti katika mikutano na wanachama wa chama chake cha zamani na katika ziara alizofanya Ulaya na Marekani kuwa “bado naamini haki ya Wazanzibari ipo na itarejea, ingawaje sijui lini itapatikana.”

Hata hivyo, kauli hiyo iliwahi kujibiwa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein akiwataka Wazanzibari kuacha kusikiliza “maneno ya propaganda kutoka kwa wapinzani” kwa kuwa katu hakuna rais mwingine atakayeongoza Zanzibar wakati yeye yupo madarakani.

Kama alivyosema Dk Shein ahadi hiyo haikupatikana hadi naamua kuachana na CUF na kuhamia ACT-Wazalendo, jambo ambalo anasema lina sababu zake.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili juzi Alhamisi, Maalim Seif anasema “yote yaliyofanywa na niliyofanyiwa ni kutaka kuzuia haki niliyokuwa ninaipigania nikiwa CUF na sasa ACT-Wazalendo”.

Kiongozi huyo aliyewahi kuwa makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), anasema alikuwa anaendelea kufuatilia ahadi yake ya kutafuta haki ya Wazanzibari hadi washindani wake wakafika mahali wakaona hakuna namna isipokuwa wamtoe Seif CUF kwa kupandikiza mgogoro.

“Ningebaki CUF, nina uhakika isingefika mwaka 2020 Wazanzibari wangepata haki yao,” anasema Maalim Seif.

“Pamoja na chama kupewa Profesa (Ibrahim) Lipumba, lakini maadam jina lipo la CUF haki ingekuja. Wakaona njia nyepesi ni kumwondoa Seif ili hata wakija wale wanaoweka shinikizo kwao, wakiuliza wanajibiwa kuwa huyu si mwanachama wa CUF tena,” anasema Maalim Seif.

Maalim Seif anasema kufukuzwa kwake CUF ni kitendo cha makusudi ili kuhakikisha ndoto yake ya kuwapatia haki Wazanzibari isifanikiwe.

Hata hivyo, Maalim Seif anasema uzuri ni kwamba Wazanzibari ni waelewa na kabla ya yeye kuchukua uamuzi wameshajua cha kufanya.

Kiongozi huyo wa zamani wa CUF, hivi sasa amejiunga na ACT-Wazalendo baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kutoa hukumu Machi 18 ikikubaliana na hoja za Msajili wa Vyama vya Siasa kumtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti halali wa CUF.

Pamoja na hatua hiyo, Seif anasisitiza, “madhumuni yote hayo ni kutuzuia tusipate haki yetu, lakini nawaambia haki haizami. Unaweza kuichelewesha tu,” anasema Seif.

Maalim Seif anahusisha ucheleweshaji wa haki hiyo na matukio wanayokumbana nayo katika siku za karibuni, kama polisi kuzuia mkutano wa ACT-Wazalendo uliopangwa kufanyika katika ukumbi wa PR, Temeke kwa madai kuwa wanachama wa CUF wanataka kufanya vurugu.

“Polisi wanakuja wanatuzuia na kutueleza kuna taarifa za intelijensia kuwa CUF wanataka kufanya vurugu. Hizi ni sababu zisizo na mashiko. Wao ni polisi, moja ya kazi zao ni kulinda usalama wa raia na kulinga mikutano ya kisiasa. Hivi kama mnawajua hao wanataka kufanya vurugu, kwa nini msiwazuie. Kazi yenu ni kutuzuia sisi au wale wanaotaka kufanya vurugu?” anahoji Maalim Seif.

Anafafanua kuwa kulikuwa na amri ya Mahakama Kuu ya kuzuia mkutano mkuu wa CUF usifanyike, lakini polisi haohao ndio walikwenda kuulinda mkutano huo.

“Kwa hali hii ni ngumu kuamini kama jeshi la polisi linatendeka haki. Hawa waliozuiwa na mahakama wasifanye mkutano mnakwenda kuwalinda. Sisi tuliojifungia ndani pahala mnatuzuia, tena tunafuatwa hadi Makao makuu ya ACT-Wazalendo,” anasema.

Maalim Seif anasema “Mbona Bashiru (Dk Ally-Katibu mkuu wa CCM) anafanya mikutano. Alipotoka (Edward –Waziri mkuu mstaafu) Lowassa Chadema kwenda CCM, Monduli kule kulikuwa na maandamano na mikutano ya hadhara polisi walichukua hatua gani?” alihoji.

Anasema jambo hilo (undumila kuwili) lipo wazi kwamba kuna watu wana haki lakini kuna wengine wana haki zaidi ya wenzao.

Mbali na hilo, Seif anasema anaunga mkono malalamiko ya ACT kwa viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na ile Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)

“Ingawa najua nchi za kusini na mashariki mwa Afrika ni tofauti za zile za magharibi. Nchi za magharibi wameendelea mbele wana misimamo... huku kwetu ni tofauti wanaheshimiana na kulindana.

“Lakini nasema kila siku wanatulaumu tunakimbilia kwa wazungu, sasa hivi tunakwenda kwa Waafrika wenzao. Jukumu letu ni kuwaeleza haya yanayotokea hapa nchini, wakiyachukua tutafurahi sana, wakiyaacha basi,” anasema Maalim Seif.

Sheria ya vyama siasa

Kuhusu Sheria mpya ya Vyama vya Siasa ambayo Rais John Magufuli ameisaini Februari 13, Maalim Seif anasema “inaathiri haki za watu sana. Kabisa kabisa na angekuwa yeye kiongozi chama angeshauriana na wenzake kwenda mahakamani.

“Hakuna njia nyingine, kwa sababu Zitto (Kabwe), Salim Bimani na Joran Bashange ulipokuwa muswada walikwenda mahakamani, lakini kukawa na mapungufu ya kisheria. Watu wajitokeze na kuipinga sheria hii,” anasema Maalim Seif.

Pia, Maalim Seif aliyepewa kadi namba moja ya ACT huku namba mbili ikisubiri mtu mwingine, anasema baada ya uamuzi wa mahakama uliompa Profesa Lipumba chama, kuna watu walidhani kuwa wafuasi wa CUF wa Zanzibar wangefanya vurugu, lakini haikutokea.

“Wao walitaka shari, ili wapate sababu kuwakamata viongozi wetu ili kuwaweka ndani hadi baada ya uchaguzi mkuu wa 2020. Lakini sisi ni vichwa, (tunatumia akili),” anasema.