Maalim Seif: Kuna njama za kutunyang’anya chama

Sunday February 10 2019

 

By Muhammed Khamis,Mwananchi [email protected]

Unguja. Katibu mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amedai kuna mikakakti inapangwa kuwapokonya chama hicho na kusema njama hizo hazitafanikiwa wala kuwavunja nguvu ya kudai haki yao mahala popote.

Hamad alitoa madai hayo kwa nyakati tofauti juzi katika mkoa wa Mjini Magharibi Unguja wakati akiwa katika ziara ya ujenzi wa chama baada ya kumaliza mkoa wa Kaskazini Unguja.

“Ninafahamu zipo njama mbalimbali zenye lengo la kunyang’anywa chama na kundi linalomuunga mkono mwenyekiti wa zamani Profesa Ibrahim Lipumba.”

“Hata kama watafanikiwa hatutanyamaza tutaendelea na harakati za kudai haki kwa misingi ya kikatiba kwani ndiyo kazi ya siasa,” alisema.

Katibu mkuu huyo wa CUF alisema anasikitishwa na wanaofanya na kuratibu mkakati huo wakishindwa kujua kuwa wanaminya demokrasia pamoja na kupalilia chuki miongoni mwa wananchi.

“Hili na mengine mengi hayataturudisha nyuma na mapambano yataendelea kama kawaida, hilo nataka kila mtu ajue ingawa njia ni nyingi,” alisema.

Awali, mkurugenzi wa uchaguzi wa CUF upande unaomuunga mkono Maalim Seif, Omar Ali Shehe aliwataka wanachama wa chama hicho kutovunjika moyo na waendelee na mshikamano kama ilivyokua siku zote.

“Yanayoendelea kutokea sasa yote ni kwa sababu ya nguvu ya chama chetu jambo ambalo limekua likiwakera baadhi ya watu na ndiyo maana wanaratibu mikakati kukihujumu,” alisema.

Akizungumza na Mwananchi juu ya tuhuma hizo, mkurugenzi wa uchaguzi na mipango wa chama hicho anayemuunga mkono Profesa Lipumba, Nassor Seif alisema kauli za Maalim Seif na wenzake hazina ukweli kwani hawana nia ya kunyang’anya chama.

Alisema kinachofanyika ni kutaka kuona Katiba ya chama hicho inafuatwa na kutekelezwa badala ya kuwaachia baadhi ya watu kukiendesha kwa matakwa na maslahi yao binafsi kwani CUF ni chama cha wananchi wote.

Advertisement