Maalim Seif, Lipumba ngoma bado mbichi

Muktasari:

Baada ya Mahakama Kuu kuwakataa wajumbe wa bodi wa kambi ya Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif na wale wa mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, kila kambi sasa imetamba kuwa na mamlaka ya kuchagua wajumbe wengine wa bodi.

Dar es Salaam. Vuta ni kuvute kati ya mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, Profesa Ibrahim Lipumba na katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Hamad umeendelea kushika kasi huku kila upande ukidai kuwa na nguvu kisheria kuunda bodi nyingine ya wadhamini.

Jumatatu iliyopita, Mahakama Kuu ilitengua uteuzi wa wajumbe wa bodi ya chama hicho kambi ya Profesa Lipumba iliyokuwa imesajiliwa na Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (Rita).

Jaji Benhajj Masoud alibatilisha uteuzi huo akisema amejiridhisha kuwa ulifanyika bila kuzingatia sheria ya muungano wa wadhamini, ambao ndiyo unasimamia usajili wa wajumbe wa bodi za wadhamini wa taasisi mbalimbali nchini.

Dk Masoud alisema hata wanachama wa chama hicho waliopendekezwa na kambi ya katibu mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad pia hawakuwa na sifa ya kuteuliwa kuwa wajumbe wa bodi kwani nao hawakuwa wamekidhi matakwa ya sheria.

Baada ya uamuzi huo, kila upande kwa nyakati tofauti umesema utateua bodi nyingine na tayari kambi ya Maalim Seif imefanya hivyo tangu juzi.

Je Rita itapokea majina ya upande upi? kaimu ofisa mtendaji mkuu wa Rita, Emmy Hudson ameiambia Mwananchi kuwa watakachoangalia ni bodi iliyoteuliwa kama imekidhi vigezo vinavyotakiwa kisheria bila kuangalia upande.

Abdul Kambaya, mkurugenzi wa habari wa CUF kambi ya Profesa Lipumba, amesema wamekubaliana na uamuzi wa Mahakama Kuu na kwamba wapo kwenye mchakato wa vikao vya juu vya taifa kuteua wajumbe kama mahakama ilivyoagiza.

Kambaya alisema chama hicho kitaitisha mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi na kazi mmojawapo itakuwa ni kuteua wajumbe wa bodi ya wadhamini.

“Rejea hukumu ya Benhajj kuhusu kutozitambua bodi za pande mbili ndiyo utajua kama tukiomba tena itakuwa na uhalali wa kisheria au kinyume chake,” alisema Kambaya.

“Upungufu ni wa kisheria na siyo ya kiutashi, kwa hiyo yakirekebishwa nina hakika bodi itakuwa na uhalali wa kisheria,” alisema.

Hata hivyo, hali ni tofauti katika kambi ya Maalim Seif ambayo inadai imeshaunda bodi hiyo.

Akizungumza na Mwananchi jana, Maalim Seif alisema kambi ya Profesa Lipumba haina Baraza Kuu la Uongozi wa Taifa.

“Mimi naamini tuliowateua sisi ndio halali. Lipumba hana Baraza Kuu la Uongozi la Taifa ambalo kwa mujibu wa Katiba ya CUF ndilo lenye mamlaka ya kuteua wajumbe.”

“Hata Mahakama iliweka wazi kuwa wajumbe walioteuliwa na Baraza la Lipumba hawakuwa halali kwa kuwa halikutimiza akidi ya wajumbe,” alisema Maalim Seif.

Maalim Seif alisema, “Baraza la Uongozi la CUF lina wajumbe 63 waliochaguliwa katika Mkutano Mkuu wa Taifa wa 2014. Hata kama wengine wamehama chama na kufariki dunia sisi tunachukulia walewale 63.”

Alisema kwa mujibu wa Katiba ya CUF kikao chochote cha chama ni lazima kihudhuriwe na wajumbe wa kikao hicho zaidi ya nusu ambayo ni 31.5 au 32.”

“Wajumbe waliohudhuria jana (juzi) ni 37, hii ni zaidi ya nusu, hivyo kikao kilikuwa halali na uamuzi wake ulikuwa halali,” alisema Maalim Seif.

“Lipumba wajumbe waliomfuata ni 13, wawili wamefariki dunia hivyo wamebaki 11 na hao wengi wao ama wamefukuzwa na Baraza Kuu halali (akiwemo Lipumba mwenyewe) na wengine wamesimamishwa (akiwemo Magdalena Khamis Sakaya). Akidi ataitolea wapi?” alihoji Maalim Seif.

Maalim Seif aliionya Rita kuwa endapo itakubali tena bodi ya Profesa Lipumba itakuwa inakiuka sheria kama Mahakama Kuu ilivyotoa hukumu yake.

Mgogoro wa CUF ulianza Agosti 2015 baada ya Profesa Lipumba kujiuzulu uenyekiti wa chama hicho akieleza kutoridhishwa na uamuzi wa vyama vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumpokea na kumpitisha Edward Lowassa kugombea urais kupitia Chadema.

Vyama vilivyounda Ukawa katika uchaguzi mkuu 2015 ni Chadema, CUF, NLD na NCCR-Mageuzi.

Baada ya mwaka mmoja, Profesa Lipumba aliibuka na kudai kurejea kwenye nafasi yake ya uenyekiti jambo lililozusha mtafaruku zaidi.

Mkutano uliofanyika Agosti 2016 ulivurugika baada ya kuhudhuriwa na Profesa Lipumba huku wafuasi wake wakipinga mchakato wa uchaguzi uliokuwa ukifanyika kujaza nafasi yake.