Maalim Seif: Shusha tanga, pandisha tanga safari ianze

Aliyekuwa katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana alipokuwa akitangaza kujiunga na chama cha ACT Wazalendo. Kushoto ni aliyekuwa naibu katibu mkuu wa chama hicho Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui. Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Maalim Seif, ambaye safari yake ya kisiasa ilianzia CCM alifukuzwa na chama hicho 1988 kabla ya kutumikia kifungo cha kisiasa jela kuanzia Mei 1989 hadi Novemba 1991.

Dar es Salaam. “Wakati ni huu, wakati ni sasa. Shusha tanga, pandisha tanga safari iendelee.” Ni tangazo la Maalim Seif Sharif Hamad kwa wanachama na wafuasi wake akiwaamuru washushe bendera za CUF na wapandishe za ACT-Wazalendo. Chama kipya walichohamia jana.

Maalim Seif jana alibadili historia yake ya miaka 27 ndani ya CUF kwa kutangaza rasmi kujiunga na chama kichanga cha Alliance for Change and Transparency maarufu kama ACT Wazalendo kilichoanzishwa 2014.

“Nawatangazia Watanzania wote na hasa wanachama wa CUF walio wengi waliokuwa wakituunga mkono kutoka kila pembe ya nchi, Tanzania Bara na Zanzibar, kwamba mimi na wenzangu tunajiunga na chama cha ACT Wazalendo. Tunawaomba na wao wote waungane na nasi kujiunga na jukwaa hili jipya kuendeleza kazi kubwa tuliyokuwa tukiifanya kupitia CUF,” alisema Maalim Seif.

Kauli hiyo ya Maalim Seif ilifuatiwa na mwitikio wa kundi la wafuasi waliokuwa nje ya ukumbi wa ofisi ya wabunge wa CUF katika eneo la Magomeni kwamba wanamfuata katika chama alichohamia.

Ofisi hiyo iliyokuwa inatumiwa na wabunge 28 wanaomuunga mkono Maalim Seif, na baada ya tangazo la kuhamia ACT Wazalendo maandishi ya CUF yaliyokuwa kwenye bango nje ya ofisi hiyo yalifutwa rasmi.

Uamuzi wa Maalim Seif aliyekuwa katibu mkuu wa CUF kwa miaka mingi ulitokana na kushindwa kesi namba 23 ya mwaka 2016 waliyoifungua kuilalamikia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kwamba haina mamlaka ya kuingilia masuala ya ndani ya chama hicho.

Maalim Seif, ambaye safari yake ya kisiasa ilianzia CCM alifukuzwa na chama hicho 1988 kabla ya kutumikia kifungo cha kisiasa jela kuanzia Mei 1989 hadi Novemba 1991.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Maalim alisema baada ya kushindwa kesi mahakamani wameona kuna haja ya kutafuta jukwaa jingine la kuendeleza mapambano ya kisiasa waliyokuwa wakiyasimamia kupitia CUF.

Maalim Seif, baada ya kutoka jela 1991 alishiriki kuanzisha CUF 1992, kwa kuviunganisha vikundi viwili vya Kamahuru kilichokuwa kikipigania demokrasia katika visiwa vya Unguja na Pemba na Civic Movement kundi la kupigania haki za binadamu la Tanzania Bara.

Kuhusu wabunge 28 wanaomuunga mkono, alisema wamewaachia uhuru wa kuamua kama watapenda kuhamia ACT Wazalendo au kubaki CUF.

Maalim Seif ambaye aliwahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Muungano wa Kitaifa ya Zanzibar (SUK), alisema wamekwenda ACT Wazalendo kama wanachama wa kawaida na hakuna aliyefuata vyeo au kuahidiwa cheo katika chama chao kipya.

“Hatua tunayochukua leo (jana) ni kuandika historia mpya ya mabadiliko ya kisiasa Tanzania, kote Zanzibar na Bara. Umma haujawahi kushindwa popote duniani. Ndivyo historia inavyoonyesha kote. Hatuna wasiwasi kwamba umma wa Watanzania nao utashinda,” alisema.

Maalim Seif ambaye amewahi kushika nafasi ya Waziri Kiongozi wa Serikali ya Zanzibar, alisema katika jukwaa lao jipya la kisiasa wao watashirikiana na vyama makini.