Maalim Seif ajiandaa kuunda safu mpya CUF

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad (kushoto) akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, baada ya Mahakama Kuu ya  Dar es Salaam kutengeua uteuzi wa wajumbe wa bodi ya wadhamini wa chama hicho. Picha na Said Khamis

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutengua uteuzi wa wajumbe wa bodi ya wadhamini ya CUF, Katibu Mkuu wa chama hicho kikuu cha upinzani visiwani Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema atateua wajumbe wengine.

“Tutafanya uteuzi mpya wa wajumbe wa bodi kwa kufuata vifungu vyote vya sheria na tutavipeleka Rita (Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi) ili isajiliwe. Ni matarajio yetu Rita itafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria,” alisema Maalim Seif.

Juzi, mahakama hiyo ilitengua uteuzi wa wajumbe waliopendekezwa Profesa Ibrahim Lipumba, mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, na kusajiliwa na Rita.

Wajumbe hao waliteuliwa na Profesa Lipumba kwa madai kuwa wajumbe wa awali walikuwa wamemaliza muda wao.

Akizungumza na Mwananchi jana, Maalim Seif alisema uamuzi huo wa mahakama umewapa nguvu wanachama wao waliokuwa wakishuhudia mvutano uliozaa makundi ndani ya chama hicho.

Tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2015, CUF imekuwa katika mgogoro uliokigawa chama hicho pande mbili; moja ya Profesa Lipumba na nyingine ya Maalim Seif zikiwahusisha mpaka wabunge, madiwani na viongozi wengine.

“Rita ni chombo muhimu katika nchi, tuna imani ya kuwa imejifunza mengi kutokana na hukumu ya jana (juzi) na italinda credibility (weledi),” alisema Maalim Seif.

Alisema uamuzi huo wa mahakama ni ushahidi tosha kuwa msajili wa Rita hakufanya kazi kwa ufanisi na kwamba hilo ni funzo kwa taasisi nyingine za Serikali katika kutekeleza majukumu yake bila kufuata msukumo.

Aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kuwa makini katika kufuata vipengele vyote vya kisheria katika utendaji kazi badala ya kufanya kwa mazoea huku akisisitiza kuwa uamuzi wa mahakama ulikuwa sahihi.

Kutokana na uamuzi huo wa mahakama, Maalim alisema wakati muafaka sasa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya uchunguzi wa kina kuhusu fedha za ruzuku akidai kwamba masuala ya fedha yalifanywa ba bodi hiyo kinyume na sheria.

Alipotafutwa jana kuzungumzia hukumu hiyo, Abdul Kambaya ambaye ni mkurugenzi wa habari na mawasiliano kwa umma wa CUF, upande wa Profesa Lipumba alisema “Pale hakuna mshindi, si sisi wala wao (CUF upande wa Maalim).”