Maalim Seif alia na ubaguzi katika ajira

Pemba. Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amedai kuna ubaguzi wa kupitiliza unaondeshwa na Serikali ya Zanzibar hususan katika ajira.

Maalim Seif alisema hayo kisiwani Pemba wakati akizungumza na viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama hicho katika mkutano maalumu uliofanyika shehia ya Ngezi wilaya ya Mkoani Pemba jana.

Alisema kwamba vijana wengi wamemaliza ngazi mbalimbali za elimu lakini wamekua wakishindwa kuajiriwa na badala yake hubaki mtaani kutokana na kile alichodai kuwa ni ubaguzi uliokithiri kwenye utoaji wa ajira.

“Hivi sasa Zanzibar ili uajiriwe unalazimika kuwa mwanachama wa CCM vinginevyo utaendelea kusota na vyeti vyako nyumbani,’’ alisema Maalim Seif

“Kama utafanya tathmini utakuta kundi kubwa la vijana waliomaliza masomo yao wengine hata miaka mitatu au minne nyuma wanaendelea kusota bila ya ajira,” alisema.

Akizungumza na Mwananchi kuhusiana na madai hayo ya Maalim Seif, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud alisema hayana ukweli kwani ajira zimekua zikitangazwa kwa mfumo maalumu wa tume ya utumishi kazini na hakuna ubaguzi wa aina yoyote unaofanyika.

“Nafasi za kazi siku zote zinatangazwa na wenye sifa huomba na kisha kufanyiwa usaili na wanaofaulu usaili huo ndiyo wanaostahiki kuajiriwa na si vinginevyo,” alisema waziri huyo.

Aboud aliongeza kwa kusema kwamba katika suala la ajira taratibu zote zenye kufuata sheria za uajiri hutumika na lengo la kupata wafanyakazi bora na wenye sifa hivyo madai ya kuwapo ubaguzi katika sekta hiyo hayana ukweli kama inavyodaiwa na kiongozi huyo wa CUF.