Maambukizi ya malaria kwa watoto Mtwara yazidi wastani wa kitaifa

Muktasari:

  • Tafiti zinaonyesha maambukizi  ya malaria kwa watoto walio chini ya miaka mitano mkoani Mtwara ni asilimia 14.8, mara mbili ya wastani  wa kitaifa wa asilimia 7.3

Mtwara. Tafiti zinaonyesha maambukizi  ya malaria kwa watoto walio chini ya miaka mitano mkoani Mtwara ni asilimia 14.8, mara mbili ya wastani  wa kitaifa wa asilimia 7.3.

Pia, vifo vitokanavyo malaria vimepungua kutoka 34 kwa kipindi cha Julai hadi Desemba hadi  vifo 23 kwa kipindi cha Januari hadi Juni, 2019.

Hayo yameelezwa na mganga mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dk Sylvia Makwe leo Jumatano Julai 17, 2019 wakati akiwasilisha taarifa kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa.

Dk Makwe amesema mkoa huo umeendelea kupambana na malaria na kwamba watu waliogundulika kuwa nao wamepungua kutoka 188,431 katika kipindi cha Julai hadi Disemba 2018 hadi kufikia 177,802 kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2019.

“Wastani wa kitaifa ni asilimia 7.3 lakini kwa Mtwara kiwango ni asilimia 14.8 wanaoongoza ni halmashauri ya Nanyamba ambao ni asilimia 19.5 ikifuatiwa na halmashauri ya wilaya ya Mtwara na Newala.”

“Tayari Serikali imenunua dawa kwa ajili ya kupulizia kwenye madimbwi ya mazalia ya mbu na tutaanza kazi ya upuliziaji rasmi mwezi ujao kwa kuwa tumeshaanza kupokea dawa,” amesema Dk Makwe.

Aidha amesema mkoa huo unatekeleza afua mbalimbali za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo kwa kutoa chandarua kwa mama mjamzito anayeanza kuhudhuria kliniki.

Mbunge wa Newala vijijini (CCM), Rashid Akbar amesema Zanzibar wameweza kupambana na malaria na hata kupunguza kiwango cha maambukizi na kuomba mkoa kuwa kupambana na mazalia ya mbu.