Maandalizi ya maonyesho ya sabasaba yaanza

Friday June 21 2019

 

By Aurea Simtowe,Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku sita kabla ya kuanza kwa Maonyesho ya 43 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba jijini Dar es Salaam nchini Tanzania ukarabati wa maeneo ya kufanyia maonyesho hayo yameanza.

Mwananchi imefika katika viwanja hivyo leo Ijumaa Juni 21, 2018 na kukuta mafundi wakiwa katika shughuli mbalimbali ikiwemo upakaji rangi, uwekaji wa mabati mapya huku wanawake wakichangamkia kazi za kusafisha mabanda.

Akizungumza na Mwananchi mmoja wa mafundi wa kupaka rangi, Khalidi Mussa amesema huu ni msimu ambao kwa kiasi huja na neema kutokana na kupata kazi nyingi za kurudishia mabati na shughuli nyingine.

“Wengine huhitaji kila mwaka kuweka mabati mapya katika maeneo yao, wengine kufanya maboresho kadhaa hivyo tunajipatia pesa, kiukweli msimu huu ni neema kwetu,” amesema Mussa

“Siyo kupiga bati tu, tunaweka salafu mpya, gympsum, kwa sababu nyingine zinakiwa zimechoka au anayeingia sasa havutiwi nazo.”

Juma Rashid ambaye ni mpaka rangi amesema kila yanapokaribia kuanza maonyesho hayo wamiliki wa maeneo hubadilika hivyo wengi huhitaji kupaka rangi ili kuifanya sehemu yake kuonekana nadhifu na inayoendana na biashara yake.

Advertisement

“Kupaka rangi ni maelewano kama chumba kimoja nafanya Sh30,000 kama ni eneo la nje ni maelewano, kipindi kama hiki kuondoka na Sh50,000 kwa siku ni kawaida sisi huwa tunaita sikukuu,” amesema Rashid

Zaitun Mbaga amesema kabla ya kuanza kwa maonyesho hayo wamekuwa wakitafuta kazi za kufanya usafi katika mabanda mbalimbali.

“Kuna kupiga deki, kufagia, kutoa buibui, kutoa nyasi katika baadhi ya sehemu zote hupatikana katika kipindi hiki ambapo kwa siku huweza kuondoka na  Sh20,000 hadi Sh30,000,” amesema Zaitun

Advertisement