Mabalozi wa nchi za Kiarabu kutibiwa macho Tanzania

Muktasari:

  • Mabalozi wa nchi sita zinazounda Jumuiya ya Mabalozi wa Nchi za Kiarabu za Algeria, Yemen, Comoro, Saudi Arabia, Palestina na Oman waliopo Tanzania  wamesema kwa sasa watapata matibabu ya macho nchini.

Dar es Salaam. Mabalozi wa nchi sita zinazounda Jumuiya ya Mabalozi wa Nchi za Kiarabu waliopo Tanzania, wamesema wataanza kupata huduma za matibabu ya nchini katika Hospitali ya Macho ya Kimataifa ya The International Eye Hospital.

Hayo wameyasema leo Jumatano Machi 20, 2019 mabalozi hao walipofanya ziara kwenye hospitali hiyo jijini Dar es Salaam. Wamesema  awali walikuwa wakisafiri kwenye nchi zao kwa ajili ya kupata huduma za uchunguzi wa macho kwa muda mrefu.

Pamoja na mabalozi hao kutoka Algeria, Yemen, Comoro, Saudi Arabia, Palestina na Oman pia wafanyakazi wa ubalozi na watumishi wa taasisi za nchi zao walikuwa wanakwenda kupata matibabu nchini mwao lakini sasa wote watahudumiwa Tanzania.

Balozi wa Yemen Fikri Al-Sakaf, amesema ziara hiyo imewawezesha kujionea jinsi hospitali hiyo inavyoweza kuwahudumia kutokana na kuwa na wataalamu na vifaa vya kutosha.

Akitoa maelezo kwa mabalozi hao meneja wa hospitali hiyo Adam Mwatima, amesema hospitali hiyo iliyoanzishwa mwaka 2014 imekuwa na msaada mkubwa kwa jamii kutokana na kujikita kwenye huduma za macho pekee.

"Kwa sasa hakuna huduma yoyote inayohusu matibabu ya macho ambayo haipatikani kwenye hospitali hii na hakuna sababu ya kwenda ng'ambo kutafuta huduma za matibabu ya macho,” amesema Mwatima.

Amesema wataalamu na vifaa vya kutosha kwa ajili ya kupima matatizo ya aina zote ya macho ikiwamo upasuaji vinapatikana hospitalini hapo.

Meneja huyo ametoa ushauri kwa jamii kuwa baadhi ya matatizo ya macho mara nyingi dalili zake hazijionyeshi haraka, hivyo ni muhimu kwa jamii kufanya uchunguzi wa mara kwa mara kubaini matatizo mapema na kuyafanyia matibabu.