Mabilionea 100 wa Magufuli walivyowaibua Zitto, Lema mitandaoni

Muktasari:

Katika mkutano wa Rais John Magufuli na wawakilishi wa wafanyabiashara kutoka Wilaya zote Tanzania uliofanyika jana Ijumaa Juni 7, 2019 Ikulu jijiji Dar es Salaam, kiongozi mkuu huyo wa nchi alieleza nia yake ya kuacha mabilioni 100 kabla ya kumaliza muda wake wa uongozi, kauli iliyowaibua wabunge, Zitto Kabwe na Godbless Lema mitandaoni


Dar es Salaam. Si unakumbuka kauli ya Rais John Magufuli aliyoitoa jana Ijumaa Juni 7, 2019 Ikulu Dar es Salaam kwamba anatamani atakapomaliza muda wake wa uongozi aache mabilionea 100 nchini Tanzania.

Kiongozi mkuu huyo wa Tanzania alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wawakilishi wa wafanyabiashara kutoka Wilaya zote nchini kwenye mkutano wa siku nzima uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali.

Katika mkutano huo wafanyabiashara hao walieleza changamoto wanazokumbana nazo na kujibiwa na Rais Magufuli, mawaziri na watendaji wa taasisi za Serikali ambao pia walieleza mikakati mbalimbali iliyofanyika na inayoendelea kufanyika ili kumaliza changamoto hizo.

Kauli hiyo ya Magufuli imeonekana kuwakuna baadhi ya wanasiasa, akiwemo mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe na mwenzake wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ambao walitumia mtandao wa kijamii wa Twitter kueleza  hisia zao kutokana na kauli hiyo ya Magufuli.

Lema alieleza kuwa hotuba ya Rais Magufuli katika mkutano huo imejaa matumaini hasa kwa kauli yake ya kuacha mabilionea 100.

“Kauli ya Rais kuwa anataka kuona Tanzania ya mabilionea100 kabla ya kumaliza muda wake wa uongozi ni kauli ya matumaini kwa nchi.”

“Kauli hii ina thamani kubwa kuliko ile ya matajiri kuishi kama mashetani. Nimemsikiliza Rais naona kama anasisitiza uwepo wa utawala bora, sheria katika ngazi zote za Serikali,” amesema Lema.

Wakati Lema akieleza hayo, Zitto amesema, “Mabilionea 100 na fukara milioni 50? Idadi ya mabilionea duniani imeongezeka katikati ya mafukara.”

“Bora kujenga uchumi unaomilikiwa na watu wengi (inclusive economy) na kuondoa umasikini. Nilisikia @hpolepole (Humphrey Polepole-Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM)  na @kitilam (Profesa Kitila Mkumbo- katibu Mkuu Wizara ya Maji) wanasema Magufuli mjamaa. Hii ndio tafsiri mpya ya Ujamaa?”

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ni miongoni mwa viongozi waliohudhuria mkutano huo.