Machozi ya familia jinsi mtoto alivyokatwa mkono Tanga

Muktasari:

Familia ya mtoto wa miaka 14 imeangua kilio katika Hospitali ya Bombo jijini Tanga baada ya kushuhudia mtoto wao, Salim Richard akikatwa mkono.

Tanga. Familia ya mtoto wa miaka 14 imeangua kilio katika Hospitali ya Bombo jijini Tanga baada ya kushuhudia mtoto wao, Salim Richard akikatwa mkono.

Salim alikatwa mkono wa kulia begani kutokana na taarifa za kitabibu kuonyesha ulikuwa ukioza na kama ungeendelea kuachwa ungeleta madhara makubwa.

Kabla ya Salim kukatwa mkono, baba mzazi wa mtoto huyo, Richard John aligoma mwanaye kukatwa mkono hadi wajomba zake watakapofika.

Salim, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Kilimangwido, wilayani Pangani alivunjika mkono Machi 8 wakati akicheza mpira na wenzake katika Uwanja wa Kijiji cha Meka, Kata ya Ubangaa.

“Mwanangu amekatwa mkono, ina maana hataweza kujimudu tena, sijui nitafanyaje maana ndiye niliyekuwa nikitegemea angeisaidia familia yangu kutokana na kuwa na bidii ya kusoma,” alisema John.

Mara baada ya kufanyiwa upasuaji huo, mtoto huyo amelazwa katika wodi ya Sokoine maarufu kwa jina la namba nane akiendelea na huduma za kitabibu.

Mtaalamu wa mifupa wa hospitali ya Bombo, Dk Jodeph Nangawe alisema kutokana na vidole pamoja na mkono kuzidi kuwa mweusi hakukuwa na njia nyingine ya kumuokoa asiendelee kupata madhara zaidi ya kumfanyia upasuaji.

“Tuliamua kumpasua lakini wazazi wake walipokuwa wakigoma kutia saini ya kuturuhusu kumpasua madhara yalikuwa yakiongezeka,” alisema Dk Nangawe.

Hadija Mashaka ambaye ni dada wa Salim akizungumza na Mwananchi, aliiomba Serikali kumsaidia ili akipona aendelee na masomo.

“Kama mnavyomuona baba mdogo kila mara analia, siyo kwamba anakufuru bali anafikiria hatima ya Salim, atasomaje kwani kutoka kijijini kwetu hadi shuleni ni mbali wanatumia baiskeli kwa muda wa saa moja, sasa itakuwaje?” alihoji Hadija.

Akielezea sababu za kukatwa mkono mwanafunzi huyo, Hadija alisema wakati akicheza mpira na wenzake Machi 8 alivunjika mkono huo wa kulia.

Alisema baada ya kuvunjika alikimbizwa hospitali ya Wilaya ya Pangani ambako Machi 9 alipewa rufaa na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Bombo na kufungwa plasta ngumu (POP) kabla ya kuruhusiwa kurejea nyumbani.

“Kama mnavyofahamu watoto wasivyojali, aliporudi akaendelea na harakati zake za kucheza na usiku alikuwa akiondoa POP kwenye kamba hadi asubuhi, kumbe mkono ulikuwa ukioza ndani kwa ndani,” alisema Hadija.

Alisema usiku wa kuamkia Alhamisi wiki iliyopita, hawakulala kwa sababu Salim alikuwa akilia sana akilalamika mkono unamuuma ndipo wakaamua kumrejesha hospitali ya Bombo ambako alipochunguzwa ilionekana lazima akatwe.

Richard, baba wa mtoto huyo akieleza sababu za mvutano huo alikiri kuwa wajomba zake waliogoma asikatwe mkono, hawakuwa wamemuona.

“Niliona kabla ya kutia saini ya kuruhusu mkono wa mwanangu kukatwa niwashirikishe upande wa wajomba zake kwa sababu mama yake mzazi alikufa tangu mwaka juzi, hivyo nikaona niwashirikishe lakini waligoma na kusema lolote litakalomtokea hawatahusika.”

Mzazi huyo alisema, hata hivyo baada ya wajomba zake kumuona walimuomba radhi na kumruhusu atie saini ili mkono ukatwe jambo ambalo hata yeye lilimpa wakati mgumu katika maisha yake.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Hospitali ya Bombo, Mwanaidi Nyarukunyo alisema kama mvutano wa familia ungeendelea walipanga kuomba kibali mahakamani.

“Alikuwa amepangiwa kukatwa mkono Ijumaa wiki iliyopita lakini kutokana na ajali ya treni, madaktari pamoja na wauguzi wote walikuwa wakishughulikia majeruhi hadi juzi ndipo alipoingizwa chumba cha upasuaji, tukaona anarudi bila mkono wa kulia” alisema Richard kwa sauti ya chini yenye kuonyesha simanzi

Hata hivyo Richard amekanusha taarifa zilizosambaa kwamba mkono wa mwanafunzi huo uliozea kwa mganga wa kienyeji na kwamba tangu alipovunjika hakuwahi kwenda sehemu nyingine zaidi ya hospitali ya Bombo na ya Wilaya ya Pangani.

Naye ofisa Ustawi wa jamii wa Hospitali ya Bombo, Mwanaidi Nyarukunyo alisema tayari ofisi yake ilianza kuchukua hatua za kuingilia kati sakata hilo baada ya kuona mwanafunzi huyo akizidi kuoza huku familia yake ikivuta katika uamuzi wa kuruhusu mkono kukatwa.

“Tulizungumza na baba yake na kumwambia kama watashindwa kuafikiana kuhusu kukatwa mkono mwanafunzi huyo tutakwenda mahakamani kuomba

ridhaa ya kisheria ili kunusuru maisha yake” alisema Mwanaidi.

Ofisa huyo alisema waliamua kuchukua hatua hiyo baada ya kupata

maelezo ya daktari aliyesema kwamba kadiri siku zilivyokuwa zikizidi

mkono huo ulikuwa ukiendelea kuoza hivyo ungehama mkononi na kuingia

katika viungo vingine.