Madereva bodaboda wasimulia jinsi wanavyowarubuni wanafunzi wa kike

Dar es Salaam. Madereva bodaboda na bajaj wamesimulia namna baadhi yao wanavyotumia usafiri huo kuwarubuni na kuwanasa wanafunzi wa kike kingono.

Tangu kuanza kwa usafiri huo nchini waendesha bodaboda na bajaj wamekuwa wakituhumiwa kuwa kati ya makundi yanayochangia tatizo la mimba shuleni.

Madereva hao walitoa simulizi hiyo jana katika mashindano yaliyoandaliwa na Jeshi la Polisi, ambapo Shirika la Hakielimu liliwaelezea wajibu wao katika kumwezesha mtoto wa kike kutimiza ndoto zake kielimu.

Simulizi ya madereva hao ilianzia kwa Hamis Juma kutoka Kinondoni aliyesema kilichosababisha aingie kwenye uhusiano wa ngono na mwanafunzi wa kidato cha pili ni mama yake kushindwa kumlipa ‘bili’ ya usafiri ya miezi miwili.

Alisema, awali mama wa mtoto huyo alimuomba awe anampeleka na kumrudisha shuleni mwanaye kila siku kwa gharama ya Sh2,000 akiahidi kulipa bili baada ya mwezi mmoja. Alisema mwezi wa kwanza ulipokwisha mama huyo hakuwa na fedha za kulipa, hivyo aliomba avumiliwe mpaka mwezi uliofuata wakati yeye akiendelea kumpeleka mwanafunzi huyo shule.

“Kumbuka ule muda nampakia yule mtoto tulikuwa tunazoeana kiasi kwamba akawa analalamika hana hela ya kutumia, basi kuna siku nikawa nampa buku au jero (Sh1,000 au 500) na mtoto tukawa tunazoeana,” alisema.

Dereva huyo alisema baadaye alijikuta amemzoea mtoto huyo zaidi na kuona kwamba ni wajibu wake kumpeleka shule, kumrudisha na hata kumpa fedha za matumizi, kisha alianza naye uhusiano wa ngono.

“Hicho ndio chanzo cha ajabu, nilipokazana kudai hela zangu kwa mama yake akawa tayari kutoka na mimi kimapenzi, nikajikuta pia naanza uhusiano na mama.”

Alisema moyoni aliendelea kujisikia vibaya, hali iliyomfanya aachane nao na kuacha pia kuwa dereva wa familia hiyo.

Alisema kwamba kwa sasa amekuwa kati ya madereva wanaowaelimisha wenzao kuachana na tabia ya kujihusisha kingono na wanafunzi.

Naye Frank Kihambe alisema wakati mwingine wanakutana na vishawishi kutoka kwa wanafunzi jambo ambalo huwawia vigumu kuepuka.

“Tunalaumiwa lakini yapo mazingira yanayotusababisha japo ni kweli kwamba sisi ndio tuna makosa,” alisema.

Kiongozi wa waendesha bodaboda Kinondoni, Abdallah Bakari alisema ni rahisi kwa kundi hilo kuwarubuni wanafunzi wa kike kwa sababu ya aina ya usafiri wanaoutumia. “Kazi hii inahusisha kuchukua namba za simu za abiria, kuwapakia wanafunzi mpaka shule wanazosoma, ni rahisi kwa dereva asiyetambua thamani ya mtoto wa kike kumrubuni,” alisema Bakari.

Mkurugenzi wa Haki Elimu, Dk John Kalage alisema tafiti nyingi zinaonyesha waendesha bodaboda wanatuhumiwa kuwarubuni wanafunzi wa kike kwa kuwapa lifti na zawadi ndogondogo na hatimaye kufanya nao ngono.

Alisema matokeo yake huwa ni baadhi ya mabinti kupata mimba za utotoni na hivyo kulazimika kukatiza masomo yao.

“Natambua vitendo hivi hufanywa tu na baadhi ya bodaboda japo vinachafua sifa ya waendesha bodaboda wote,” alisema Kalaghe.

Alisema mkakati wa elimu kwa mwaka 2017-2021 ni kuhakikisha vikwazo vyote vinavyokwamisha elimu kwa mtoto wa kike vinaondolewa kikiwamo hicho cha bodaboda.

Kamishna msaidizi wa Polisi, Abdi Isango alisema huenda waendesha bodaboda wanajihusisha na vitendo hivyo kwa kusahau kuwa ni kosa la jinai.

Alisema kuna mashindano yanayohusu bodaboda na bajaj ambayo yataendeshwa nchi nzima huku ujumbe ukiwa ‘zuia ajali, tii sheria, okoa maisha na suala la kuwalinda watoto wa kike shuleni.