Madereva wa mabasi makubwa waiburuza Sumatra mahakamani

Muktasari:

  • Mwanasheria Mkuu wa Uwamata, Frank Kisanga amesema kesi hiyo imefunguliwa juzi

Dar es Salaam. Chama cha Madereva Tanzania (Uwamata), kimeiburuza mahakamani Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (Sumatra), pamoja na mambo mengine wakipinga hatua ya mamlaka hiyo kuwatoza faini kubwa,   kuwakamata na kuwanyang’anya leseni kinyume cha Sheria ya Usalama Barabarani.

Sambamba na kesi hiyo ya msingi, pia wamefungua maombi ya zuio wakiiomba mahakama hiyo iizuie Sumatra kuendelea kuwatoza faini kwa makosa mbalimbali ya barabarani, mpaka kesi yao ya msingi itakapoamriwa.

Akizungumza na Mwananchi jana Jumanne Aprili 14, 2019 baada ya kikao cha wadau wa usafiri nchini na waandishi wa habari kuhusu tamko la usitishwaji wa mgomo uliokuwa ukitangazwa na watu wasiojulikana kwenye mitandao ya jamii,   Kisanga alisema kesi hiyo imefunguliwa juzi.

Kisanga alisema kesi hiyo imefunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam juzi na Katibu wa chama hicho, Abdallah Lubala  dhidi ya Sumatra, wakiomba pamoja na mambo mengine iamue kuwa wanapofanya kosa waadhibiwe kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani.

Alisema Sumatra imekuwa ikiwakamata madereva hao kwa makosa mbalimbali ya barabarani na kuwatoza faini kubwa kwa kutumia kanuni za Sumatra, kuwakamata na kuwaweka mahabusu kwa kushirikiana na baadhi ya polisi na wakati mwingine hata kuwanyima dhamana.

Kisanga alifafanua kuwa dereva anapaswa  ashtakiwe na kuadhibiwa kwa sheria za usalama barabarani, lakini kwa sasa anaadhibiwa kwa kutumia kanuni za Sumatra ambazo alisema zinapingana na sheria  ya usalama barabarani.

 “Kwa hiyo katika kesi hiyo wanachokiomba ni kwamba wanapokosea waandhibiwe kwa mujibu wa sheria zilizowekwa na Bunge,” amesema.

Alisisitiza kuwa si kwamba wanatetea makosa wala madereva wanapofanya makossa, bali waadhibiwe kwa utaratibu huo wa sheria.

Alibainisha kwamba tatizo hilo limekuwa kubwa  Morogoro ambako imefikia dereva anapofanya kosa la kuendesha kwa mwendokasi anaandikiwa faini mpaka ya Sh1 milioni kwa dereva anayepewa posho ya Sh25,000 au Sh30,000 na anatakiwa alipe nusu yake papo hapo.

Alisema dereva akishindwa wanazuia gari na yeye mwenyewe na kwamba, wakati mwingine kuna baadhi ya askari wanaoshirikiana nao wanaamriwa kuwakamata na kuwaweka mahabusu na   kuwanyima dhamana wananyimwa.

Awali, Kisanga alibainisha kuwa Sumatra makosa mengine ambayo wamekuwa wakiyakagua ni mikanda au uchakavu wa gari ambayo yamo kwenye sheria ya usalama barabarani.

“Wao wangekagua masuala kama ya tiketi au vibali vya njia, hayo ndio wanayohusiana nayo na hata trafiki (askari wa usalama) hatujaona wanaingia kwenye masuala kama haya. Kwa hiyo waache mamlaka husika itende kama jinsi sheria inavyotaka,” amesema.

Awali, Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kilipiga marufuku mgomo wa madereva hao ambao ulikuwa unapangwa kufanyika kuanzia leo na kuwataka madereva hao kuendelea kutoa huduma wakati madai yao yakishughulikiwa.

Amri hiyo za zuio la mgomo huo ilitolewa na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Muslimu kufuatia kuwapo kwa taarifa za mgomo huo ambazo zilikuwa zikisambazwa katika mitandao ya kijamii kuanzia Jumapili.

Muslim alisema mgomo huo ni batili na jinai kwa kuwa haujafuata taratibu za kisheria na kwamba mambo wanayoyalalamikia tayari yapo mahakamani.