MAWAIDHA YA IJUMAA: Madhara ya pombe kiimani na kijamii

Pombe kwa tafsiri tuliyoizoea ni kile kinywaji ambacho kinaifunika akili ya mwanaadamu isifanye kazi yake ya kawaida.

Pombe haina kazi kubwa inayokusudiwa wakati wa kunywewa zaidi ya kuizuia na kuisimamisha akili ya mwanaadamu isifanye kazi yake ya kawaida.

Kutokana na umuhimu wa akili na ukweli kuwa kazi kubwa ya pombe ni kuharibu akili, mtaalamu mmoja aliwahi kusema (nanukuu): “Lau ingekuwa akili inauzwa watu wangeshindana katika kupandisha bei, lakini maajabu ni mtu kununua kwa mali yake pombe ili aharibu akili”.

Mwanaadamu anaihitaji akili ili ajiandae kwenda kazini asubuhi, afike salama kazini kwake na aweze kutekeleza majukumu yake ya kazi na ndio maana mfanyakazi yeyote hata wa hicho kiwanda cha pombe akikutwa amekunywa pombe kazini anafukuzwa kazi.

Akili pia inahitajika nyumbani ili kujua hali za watoto na familia kwa ujumla vipi wameshinda, ni nani hakwenda shule na kwa nini? Akili inahitajika ili kudumisha uhusiano kati ya mume na mke nyumbani kwani aliyelewa hana uwezo wa ‘kuboresha’ ndoa.

Akili inahitajika muda wote ili kupokea taarifa mbalimbali ikiwamo za dharura kama vile kuuguliwa, kufiwa, mafuriko, moto, maradhi ya mlipuko, majanga na kadhalika.

Mwanaadamu anapokosa akili anageuka kuwa muovu na mbaya zaidi ya mnyama. Kwa muktadha huo, hakuna mwanya, nafasi wala nukta hata moja ambayo mwanaadamu yuko huru kiasi cha kutoihitajia akili.

Kwa upande wa kiimani, pombe ina madhara makubwa sana. Kwanza ni kupinga katazo la Mwenyezi Mungu waziwazi ambalo linamtaka mwanaadamu asinywe pombe.

Mwenyezi Mungu anasema: “Enyi Waumini! Hakika pombe na kamari na masanamu na kupiga ramli ni uchafu, jiepusheni”.

Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema: “Mwenyezi Mungu ameilaani pombe na mwenye kuinywa na mwenye kumuandalia (mnywaji) na mwenye kuiuza na kuinunua na mwenye kuikamua na yule anayekamuliwa (ili ainywe) na mwenye kuibeba na yule anayebebewa (ili apelekewe akainywe”.

Kupitia hadithi hiyo tunajifunza kwamba pombe inaathari kundi kubwa sana kwa kulaaniwa na Mwenyezi Mungu.

Pili, mnywa pombe akifa hali ya kuwa kalewa haingii peponi. Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema: “Watu watatu hawatoingia Peponi: mwenye kudumisha kunywa pombe, mwenye kuukata udugu na mwenye kuuamini uchawi (anaamini kwamba uchawi una nguvu kuliko Mwenyezi Mungu)”.

Kwa upande wa kijamii, mnywa pombe anawaudhi wengine kwani anapiga kelele bila ya staha, anajisaidia popote, anaudhi wapiti njia, akienda haja wenzake wanakereka na kuudhika chooni na kama anayo taaluma fulani ambayo jamii inaihitaji anaiudhi jamii kwani hawezi kuitoa.

Mnywa pombe anasababisha ajali pindi akiendesha hali ya kuwa kalewa. Pia mnywa pombe anapogombana na mkewe au mumewe au familia yake nyumbani anaiudhi jamii yote inayomzunguka. Mnywa pombe anaweza kulala ambapo hapakuandaliwa hivyo anawaudhi wengine.

Kwa upande wa kifamilia, mnywa pombe anamuudhi mkewe anayemsubiri ili wajadiliane mambo ya familia lakini yeye anarudi amelewa kiasi kwamba hawezi hata kumsahihisha mtoto wake anayekosea.

Mnywa pombe hana msaada wowote kwa matatizo yoyote yanayotokea usiku nyumbani kwake. Pia mnywa pombe akiingia sehemu ya haja hawezi kufuata utaratibu, anajisaidia popote na kuacha harufu mbaya inayo kera.

Pamoja na madhara yote hayo, ni vyema Serikali ikaanzisha mchakato wa tafakuri maalum ya kitaifa juu ya pombe ili jamii itafakari na ichangie fikra juu ya madhara ya pombe kitaifa.

Ni madereva wangapi wamesababisha ajali kutokana na unywaji wa pombe mpaka Serikali imelazimika kununua vifaa vya kuwapima ulevi? Ni wanaume wangapi wamewapiga wake zao baada ya kulewa na wengine kuwaua kabisa?

Ni wafanyakazi wangapi wamefukuzwa kazi kwa sababu ya pombe? Ni viongozi wangapi wamenyimwa nafasi muhimu pamoja na uwezo walio nao kutokana na pombe? Ni kinamama wangapi wamewatelekeza watoto wao ili waende vilabuni wakanywe pombe?

Baada ya tafakuri hiyo ambayo nina hakika Serikali inazo takwimu kadhaa, tufikirie kutunga sheria juu ya uharamu wa pombe Tanzania. Tuiombe Serikali ianze mchakato wa kutunga rasimu ya sheria hiyo na nina hakika ikifika bungeni wabunge wengi watakubali hoja na lile pato linalotokana na pombe tutalifidia kwa neema nyengine nyingi tulizobarikiwa na Mwenyezi Mungu.

Tanzania tumebarikiwa kuwa na Bahari ya Hindi, maziwa makubwa matatu ambayo ni Victoria, Tanganyika na Nyasa, tuna Mlima Kilimanjaro na Mbuga mbalimbali za wanyama, tuna madini mengi mno, tuna ardhi yenye rutuba inayokubali kilimo, tuna viwanda kadhaa na kadhalika. Yeyote anayeamini kwamba bila ya pato la pombe tutakufa njaa, huyo si Mtanzania na haijui Tanzania kiuchumi na hamjui Mwenyezi Mungu. Mwandishi wa makala haya ni Mwenyekiti wa Arrisaalah Islamic Foundation. 0754 299 749/ 0 784 299 749