Maelekezo manne ya Majaliwa kwa vituo vya kulea watoto yatima

Muktasari:

  • Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa maelekezo manne yatakayosaidia taasisi zinazojishughulisha na utoaji wa huduma za kuwalea watoto wanaoishi katika mazingira magumu wakiwemo yatima

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa maelekezo manne yatakayosaidia taasisi zinazojishughulisha na utoaji wa huduma za kulea watoto wanaoishi katika mazingira magumu wakiwemo yatima.

Majaliwa ambaye pia ni mbunge wa Ruangwa ametoa kauli hiyo jana  Jumapili Mei 26, 2019 aliposhiriki hafla ya futari iliyofanyika kwenye viwanja vya Karimjee  iliyoandaliwa na  Mboni Masimba kupitia kipindi chake cha kuelimisha na kuburudisha cha The Mboni Show.

Majaliwa amesema  maelekezo hayo yatasaidia uendeshaji wa taasisi hizo katika kufuata na kuzingatia utoaji huduma kwa watoto hao kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya Namba 21 ya mwaka 2009.

Ameyataja maelekezo hayo kuwa ni  ofisa wa ustawi wa jamii lazima ahusike moja kwa moja kusajili mtoto katika makao au taasisi ya kulelea inapoanzishwa katika eneo fulani.

" Lengo ni kuhakikisha watoto wenye sifa ndio wanaostahili kusajiliwa na kukaa kwenye makao au taasisi husika," amesema Majaliwa.

Jambo la pili, amesema makao au taasisi hizo kuhakikisha mtoto anawekea utaratibu maalumu utakaomfanya aondoke kwenye eneo na kuunganishwa na ndugu au familia yake ambayo itaridhia kumchukua.

Majaliwa amesema jambo jingine ni wamiliki wa maeneo hayo kuwaruhusu maofisa wa ustawi wa jamii kufika kwenye maeneo yao na wao waeleze changamoto zao ili wajue namna ya kuzitatua sanjari kuwakubalia kufanya ukaguzi.

Kwa mujibu wa Majaliwa, jambo la nne ni taasisi na makao kuandaa utaratibu wa taarifa za kila mwezi za watoto na fedha wanazochangiwa  ili zijulikane na jamii inayowazunguka.

"Hatua hii itasaidia kujenga imani na wachangiaji ili mpate mchango zaidi. Lengo jingine ni kuhakikisha wazo la  kuanzisha taasisi na makao linafuata taratibu kwa maslahi ya Taifa," amesema Majaliwa.

Katika hatua nyingine, Majaliwa aliwaonya baadhi ya wamiliki wa maeneo ya kulea watoto kuacha tabia ya kuwabadilisha dini watoto hao kinyume cha sheria sanjari kuwanyanyasa na kuwafanyia vitendo vya ukatili.

Awali Masimba alimweleza Majaliwa kuwa hafla hiyo imeshirikisha watu mbalimbali wakiwemo watoto yatima 325 kutoka  vituo sita vinavyowalea na kwamba mchakato huo ni sehemu ya kurudisha shukrani zao kwa jamii.