Mafuriko yaua watano, 2,570 hawana pa kuishi

Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Masebe Kata ya Mwaya, Wilayani Kyela mkoani Mbeya, Augusta Mwakalambile akianika madaftari yake baada ya nyumba yao kujaa maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na kusababisha mafuriko. Picha na Godfrey Kahango

Kyela. Mvua zinazoendelea kunyesha wilayani Kyela, Mbeya zimesababisha vifo vya watu watano na wengine 2,570 kutoka kata saba kukosa mahala pa kuishi baada ya kaya 438 kubomolewa na nyingine kusombwa na maji kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.

Mbali ya vifo hivyo, nyumba nyingi zimebomoka, vyakula, nguo na mifugo vimesombwa na maji na uongozi ya Wilaya ya Kyela umewahifadhi wananchi kwenye kambi maalumu hadi pale mvua zitakapopungua. Hadi sasa kuna kambi 14 kwenye makanisa na shule.

Ofisa Tawala wa Wilaya ya Kyela, Salome Magambo alisema wananchi walioathirika zaidi na mafuriko hayo ni wa kata za Ikama, Mwaya, Matema, Katumba Songwe, Bujonde, Talatala na Kajunjumele.

“Hizi mvua zimesababisha maafa makubwa, watu watano hadi sasa wamefariki kutokana na mafuriko haya, lakini kati ya watu hao 2,570 walioathirika, watu 1,990 ndio tuliowahifadhi kwenye kambi hizo 14 tofauti na wengine. Bahati nzuri walikwenda kujihafadhi kwa ndugu zao ambao nyumba zao zipo kwenye mwinuko na wengine wamekuja huku mjini Kyela kwa ndugu zao,” alisema akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Claudia Kitta.

“Tunaendelea kuwapatia misaada muhimu ya kibinadamu ikiwamo, vyakula na dawa na tunashukuru wadau mbalimbali wanaendelea kujitokeza kusaidia wale ndugu zetu walioathirika.”

Alisema shule saba za msingi na sekondari zimefungwa kwa muda hadi pale hali itakapotengamaa na wanafunzi wanaokwenda ni wa darasa la saba na kidato cha nne kwa kuwa wapo kwenye mitihani.

Alisema ‘Unajua mafuriko haya sisi huku tunayapata kutokana na mvua zinazonyesha kwenye milima ya Rungwe na sisi huku tupo bondeni hivyo maji yote yanatiririka kwenye mito ukiwamo Mto Mbaka unaomwaga maji yake ziwa Nyasa. Hivyo mto huo umejaa mno na maji kuanza kupasua njia’.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Masebe, Saimon Mwakubuja alisema hadi sasa wananchi wake wanaendelea kuhifadhiwa kwenye shule ya msingi Masebe na wengine kanisani kwa muda wa wiki moja sasa lakini pia hawana aina yoyote ya chakula wala nguo za kuvaa kutokana na mali zao kusombwa na maji na nyingine nyumba kubomoka kabisa.

Alisema, ‘Hali iliyopo ni mbaya sana hadi sasa ng’ombe watano wameokotwa wamekufa, lakini wengi zaidi hawaonekani walipo, vyakula na vitu vingine vyote vilisombwa na maji. Kwa sasa huwezi kuuona mto Mbaka ni upi kutokana na kuja na kuanza kujitafutia njia’.

Mkazi wa Kijiji cha Masebe ambaye amejihafadhi kwenye Shule ya Msingi Masebe Rehema Itenda alisema ‘Huku kwetu maji yalikuja ghafla tu usiku wa Mei 4 mwaka huu. Usiku tumelala tukaona vyombo vinaelea na sisi tukijikuta tupo juu ya maji.

Tukaanza kuhangaika kutoka nje na kukimbia na watoto, hadi kunakucha tukawa tupo kwenye wakati mgumu, vyakula vyote, nguo, vyombo, na mifugo yote ikasombwa na maji. Na hapa tulipo tumejihifadhi tu shuleni lakini hatuna chakula, tunategemea misaada ya tu ya wasamaria wema’.

Mkazi wa Kitongoji cha Lugoje Kijiji cha Masebe, Totala Mwakalambile alisema mafuriko hayo mbali na kuathiri nyumba na vyakula vilivyokuwa ndani lakini mashambani mazao yote yamesombwa na maji hivyo wanaiona janga la njaa litakalowakumba.

Alisema “Huko shambani hali ni tete, kwani hakuna mwenye uhakika kama atavuna, hadi sasa mipunga yote imezama kwa maji na hatujui kama maji yakipungua basi mpunga utaonekana au ndio umeng’olewa kabisa. Lakini barabara zetu kama mnavyoziona zimefumuliwa na maji kila kona, tunaiomba Serikali ianze kuchukua hatua za haraka kutunusuru sisi wananchi wake’.