Magari 166 yaliyonunuliwa ndani ya miaka mitano bado hayajaletwa

Dar es Salaam. Jumla ya magari 166 yaliyoagizwa na taasisi nne za Serikali na kununuliwa na Wakala wa Ununuzi wa Serikali (GPSA) ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita, hayajaingia nchini.

Hayo yamo katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka 2017/18 iliyochunguza ununuzi wa magari ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mamlaka ya Hifadhi za Ngorongoro (NCAA), Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Mkaguzi huyo anasema baadhi ya magari hayo yaliagizwa mwaka wa fedha 2014/15. Kati ya magari 31 yaliyoagizwa na NCAA, ripoti inaonyesha ni mawili tu yalifika ndani ya miezi mitatu ya mkataba. Magari 29 yaliyobaki hayajaletwa nchini mpaka Januari wakati ukaguzi ulipofanyika.

Ripoti inasema NCAA iliyagiza magari hayo kwa awamu. Magari 12 yaliagizwa Mei 2015 na sita yakaagizwa Mei 2016 na manne Juni 29, 2017, lakini bado hayajafika.

Taasisi nyingine ambazo magari yake hayajafika ni Halmashauri ya Jiji la Arusha iliyoagiza magari Aprili 2015, Tanroads iliyoagiza magari tisa Mei 2015 na mengine 28 yaliyoagizwa Machi 2017 na mengine 16 ya Februari 2018 pamoja na matatu Septemba 13, 2018.

Taasisi nyingine ambazo ziliagiza magari wakati huo ni Tanapa iliyoagiza magari 18 Januari 2016 na mengine 53 Desemba 2016 na 33 yaliyoagizwa Julai 2017. Vilevile, kuna magari 33 ya TPA yaliyoagizwa Julai 2017.

Ripoti hiyo imetaja sababu za ucheleweshaji huo kuwa ni pamoja na kutokuwepo kwa kiwango cha muda maalum wa kushughulikia uagizaji huo wa magari hayo.

“Baada ya kufanya uchambuzi wa kina wa mpango mkakati, kanuni mpya na viashiria, timu ya ukaguzi iligundua kwamba GPSA haijaweka vipimo mahsusi kushughulikia kazi hiyo ikiwa kupokea na kuandaa maombi na kufikisha kwa wateja,” imesema ripoti hiyo. Sababu nyingine ni uwekaji wa maombi usiofuatana kati ya wateja na GPSA.

Ripoti hiyo pia imetaja madhara ya kuchelewesha magari hayo kuwa pamoja na kuongeza gharama kwa taasisi hiyo kwa kuwa hulazimika kutafuta njia nyingine kupata usafiri ikiwa ni pamoja na kukodi kama hawana njia mbadala.

Hasara nyingine ni kuongeza mzigo kwa magari yaliyopo na wafanyakazi, huku pia magari yakiharibika kutokana na matumizi yaliyopitiliza na kusababisha taasisi hizo kushindwa kufikia malengo yake.

Mwaka jana, katika ziara yake ya kushtukiza bandarini, Rais John Magufuli alikuta magari yaliyoagizwa na Jeshi la Polisi tangu mwaka 2015 yakiwa bandarini na hivyo kuiagiza Wizara ya Fedha, Mamlaka ya Bandari na Jeshi la Polisi kukaa pamoja kuangalia jinsi ya kuyatoa magari hayo.

Ripoti hiyo pia imebaini kuwa GPSA haifuati Sheria ya Manunuzi ya Umma inayotaka kushindanisha wazabuni kabla ya kumteua mmoja kwa ajili ya kuagiza magari.