Magufuli: Jengo la Terminal III ni la Watanzania

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amefungua jengo la tatu la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) akibainisha kuwa ni mali ya Watanzania

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amefungua jengo la tatu la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) akibainisha kuwa ni mali ya Watanzania.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Agosti Mosi, 2019 wakati akizindua jengo hilo lililofungwa kamera 296 za usalama.

Jengo hilo litakuwa likitumiwa na abiria wanaokwenda na kutoka nje ya Tanzania.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi amesema kukamilika kwa jengo hilo kutachangia kuboresha huduma za usafiri wa anga nchini.

Amesema katika majengo mawili yaliyopo hadi sasa, moja lina uwezo wa kuhudumia abiria 500,000 na la pili abiria milioni 1.5 huku hilo la tatu likiwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni sita kwa mwaka.

“Jengo hili nimeambiwa linaweza kuhudumia abiria 2,800 kwa saa, haya ni maendeleo makubwa sana kwa Taifa na limegharimu zaidi ya Sh710 bilioni. Ninamshukuru Jakaya Mrisho Kikwete (rais mstaafu) kwa kuanzisha mradi huu,” amesema Rais Magufuli.

Huku akisisitiza kuwa jengo hilo pamoja na miradi mingine mikubwa nchini ni ya Watanzania amesema, “Watanzania tunaweza kama tutaamua na kuthubutu, tumeamua na tunaendelea kuamua. Ni heshima ya mradi huu uende kwa Watanzania wenyewe na miradi yote inayotekelezwa ni ya Watanzania.”

“Nataka kuwaambia kujiita masikini tukutupe, nchi yetu ni tajiri ila tulitaka kuaminishwa na watu waliotaka kujimilikisha. Kila palipo na nia Mungu yupo na ndugu zangu Watanzania Mungu yupo pamoja na sisi.”

Jengo hilo lilianza kujengwa mwaka 2013 na awali ulipangwa kutekelezwa kwa Sh705.3 bilioni lakini kutokana na kubadilika kwa taratibu za kikodi, mchoro wa mradi , gharama ya mradi huo iliongezeka kwa Sh85.3 bilioni.

Wakati mradi unaanza ulitarajiwa ungekamilika Desemba 2017, baadaye ukaongezewa mwaka mmoja hadi Desemba 2018, lakini haukukamilika badala yake umekamilika Mei, 2019.

Kampuni iliyotekeleza mradi huo ni BAM International ya Uholanzi ambayo ndiyo iliyofanya kazi za ukandarasi na kampuni ya Arab Consulting Engineers (ACE) ya Misri, ilifanya kazi za ushauri.