Magufuli; Mashindano ya Quran yapaswa kushirikisha nchi zote za Afrika

Sunday May 19 2019

 

By Aurea Simtowe,Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema japo alikuwa haelewi kilichokuwa kikisomwa katika Quran lakini sauti zilikuwa zikimvutia hasa  ya mwanamama mmoja ndiyo imemchanganya zaidi huku akisema angekuwa mtoa maksi wangeshinda wote.

Amesema mashindano hayo sasa yanapaswa kuongezwa kutoka nchi 18 zinazoshiriki sasa na kuwa ruksa kwa nchi zote za Afrika.

Rais Magufuli amesema hayo leo Jumapili ya Mei 19, 2019 katika Mashindano ya 20 ya kusoma na kuhifadhi Quran  Afrika yaliyofanyika katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Amesema wakati Quran zikisomwa Mufti alikuwa akijitahidi kumtafsiria maana alikuwa haelewi kinachozungumzwa zaidi ya kusikia sauti nzuri.

“Ningekuwa mtoa maksi wote wangeshinda lakini sauti ya yule mwanamama imenichanganya zaidi, ninaambiwa anatoka Pwani hii inadhihirishwa Wakwere wana sauti Nzuri, sasa sifahamu dada yake na Kikwete kama naye ana sauti kama hiyo.” Amesema Magufuli.

“Napenda kuwapongeza waandaaji wa mashindano ya Quran na kwa wingi wa watu waliojitokeza katika mashindano haya Mungu atusamehe dhambi zetu.” Amesema

Advertisement

Amesema kutokana na kile kinachofanyika sasa na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Saudi Arabia anafikiri kuna umuhimu wa kumualika mfalme wa Saudi Arabia kuja kuitembelea Tanzania.

“Nina imani Mheshimiwa Waziri utafikisha maombi haya na yatajibiwa.” Amesema Magufuli.

Advertisement