Magufuli afuta kodi ya ardhi kwa madhehebu ya dini

Rais wa Tanzania, John Magufuli

Muktasari:

  • Kuanzia Julai mosi mwaka 2019 makanisa yote nchini hayatatakiwa kulipa kodi ya ardhi kama zamani baada ya Rais kufuta kodi hiyo kwa madhehebu yote.

Mbeya. Rais wa Tanzania, John Magufuli amefuta kodi ya ardhi kwa madhehebu ya dini nchini kuanzia mwaka wa fedha ujao 2019/2020.

Hatua hiyo imetangazwa leo Jumapili Januari 27, 2019 na waziri wa Ardhi, William Lukuvi jijini Mbeya wakati wa ibada ya kuwawekea wakfu viongozi wa Jumuiya Kuu ya Kanisa la Kibaptisti Tanzania (BCT).

Lukuvi amesema Rais Magufuli ameiagiza wizara hiyo kutoyatoza kodi madhehebu ya dini kwa sehemu ambazo zimeandaliwa kwa ajili kutoa huduma za maombi.

"Rais ameagiza kuanzia Julai mosi mwaka wa fedha ujao madhehebu ya dini yasilipe kodi ya ardhi kwa maeneo ambayo huduma za maombi zinatolewa si sehemu ambazo kuna miradi ya kuingiza fedha ambayo tunajua madhehebu mengi yameanzisha," amesema Lukuvi.

Lukuvi amefafanua maagizo hayo tayari yametolewa kwa makamishna wa ardhi wa kanda na mikoa pamoja na maofisa ardhi wa majiji, manispaa na halmashauri nchi nzima.

Hata hivyo, Lukuvi ametoa nafasi ya kukutana na viongozi wa dini ambao wana migogoro ya ardhi kwenye maeneo ambayo wanatoa huduma.

"Najua kuna migogoro mingi kwenye maeneo ambayo mnatoa huduma hivyo nawakaribisha ofisini kwangu Dodoma na kama migogoro itakuwa mikubwa nitafika mpaka eneo la mgogoro," amesema Lukuvi.

“Wizara yangu imepewa jukumu la kutatua migogoro ya ardhi kabla ya mwaka 2020 na tusipotatua migogoro ya dini inaweza kupelekea uvunjifu wa amani nchini hivyo hatutaki kuifuga migogoro iliyopo,” amesema.

Awali, askofu wa kanisa la Baptisti nchini, Arnold Manase amesema kanisa lake ni moja ya madhehebu yanayoongoza kuwa na migogoro ya ardhi na baadhi ya waumini wa kanisa hilo.

"Kwa kuwa waziri mwenye dhamana upo naomba nafasi nije ofisini kwako nikueleze migogoro iliyopo ndani ya kanisa langu ili uangalie namna ya kuitatua maana migogoro imekithiri mpaka kufikia hatua ya kujenga makundi miongoni mwa waumini," amesema Manase.