Magufuli akutana na bosi wa zamani wa Usalama wa Taifa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia jambo na Mzee Apson Mwang’onda Mkurugenzi Mkuu Mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa, wakati wanaagana mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam.Disemba 6,2018.


Muktasari:

Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na mkurugenzi mkuu mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa,  Apson Mwang’onda, Ikulu Dar es Salaam


Dar es Salaam. Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na mkurugenzi mkuu mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa,  Apson Mwang’onda, Ikulu Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Desemba 6, 2018 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa inaeleza kuwa baada ya mazungumzo hayo Mwang’onda amemshukuru Rais Magufuli kwa kukubali ombi lake la kumuona.

Inaeleza kuwa Mwang’onda amepongeza uongozi wa Rais Magufuli unaochochea kasi ya maendelo hususani katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.

Mwang’onda ameitaja baadhi ya miradi mikubwa ya maendeleo kuwa ni mradi wa uzalishaji wa umeme katika mto Rufiji (Stieglers Gorge), ujenzi wa madaraja na barabara ambazo licha ya kurahisisha usafiri zitasaidia kuondoa msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.

“Mabadiliko ni makubwa sana ambayo yametokea , kuna miradi mikubwa mingi inafanyika sasa hivi kwa hiyo mabadiliko ni makubwa kusema kweli na yote hayo ni kwa manufaa ya nchi. Kwa hiyo ninachoweza kusema amefanya kazi kubwa kwa maendeleo ya nchi,” amenukuliwa Mwang’onda.