Magufuli amteua Bashe kuwa waziri, atengua uteuzi wa Makamba

Muktasari:

Rais wa Tanzania,  John Magufuli ametengua uteuzi wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira),  January Makamba huku akimteua mbunge wa Nzega Mjini,  Hussein Bashe kuwa naibu Waziri wa Kilimo.

Dar es Salaam.  Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Jumapili Julai 21, 2019 amefanya mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri kwa kuwateua mawaziri wapya mawili.

Taarifa ya mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa inaeleza kuwa mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe ameteuliwa kuwa naibu Waziri wa Kilimo kuchukua nafasi ya Innocent Bashungwa ambaye hivi karibuni ameteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda.

Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi,  Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kuchukua nafasi ya January Makamba ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Pia, Rais Magufuli amemteua Balozi Martin Lumbanga kuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya mamlaka ya udhibiti wa ununuzi wa umma (PPRA).

Balozi Lumbanga  ameteuliwa kushika nafasi hiyo kwa kipindi cha pili. Taarifa hiyo inaeleza kuwa uteuzi huo umeanza leo.