Magufuli ataja sababu za kumng’oa bosi TCRA

Rais wa Tanzania, John Magufuli 

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Ijumaa ameshuhudia makabidhiano ya Mfumo wa kusimamia uwazi katika mawasiliano ya simu (TTMS) katika hafla iliyofanyika kwneye ofisi za Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) jijini Dar es Salaam na kueleza sababu za kumuondoa aliyekuwa bosi wa TCRA, Dk Ally Simba

 


Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema wakati anaingia madarakani alikuwa haridhishwi na utendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa sababu nchi ilikuwa inaibiwa sana huku baadhi ya viongozi wa Serikali wakishiriki katika jambo hilo.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Ijumaa Januari 18, 2019 katika hafla ya makabidhiano ya Mfumo wa kusimamia uwazi katika mawasiliano ya simu (TTMS) iliyofanyika katika ofisi za TCRA jijini Dar es Salaam.

Amesema kutokana na jambo hilo aliamua kuutafuta mkataba halisia ambao ulifutwa hususani kipengele cha kukusanya fedha katika makampuni yanayotoa huduma za mawasiliano hakikuwepo.

 “Nikatumia mbinu zangu na vyombo vya ulinzi vya Tanzania vinavyojua kuchokoa vizuri sana mkataba original ukapatikana na nikatengua uteuzi wa aliyekuwa mkurugenzi wa TCRA (Dkt Ally) Simba na kupeleka mapendekezo bungeni ili kukirudisha kile kipengele,” amesema Rais Magufuli.

“Kiliporudishwa tukamuambia mkandarasi kurudi kutimiza kilichopo katika mkataba wake na walielewa na kurudi kufanya kilichomo ndiyo maana leo tunakabidhiwa,” ameongeza.

Pia, kutokana na utendaji kazi mzuri ulioonyeshwa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba, Rais Magufuli amemwongezea miaka mitano katika mkataba wake ili aendelee kusimamia kikamilifu mamlaka hiyo