Magufuli ataja vikwazo vya biashara Tanzania

Muktasari:

Uwepo wa taasisi nyingi zinazofanya shughuli moja zimetajwa kudumaza ukuaji wa biashara Tanzania huku nyingine zikishindwa kufanya vizuri kutokana na kukosa fedha kutoka serikalini


Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema uwepo wa taasisi nyingi zinazofanya shughuli za aina moja umekuwa ni chanzo cha kukwamisha ukuaji wa biashara nchini.

Mkuu huyo wa nchi amesema hayo leo Ijumaa Juni 7, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam katika kikao chake na wafanyabiashara kutoka wilaya zote nchini chenye lengo la kuangazia changamoto zinazoikabili sekta ya biashara.

Magufuli amesema uwepo wa utitiri huo wakati mwingine umekuwa kikwazo kuanzisha na kuendesha shughuli za biashara Tanzania huku akitolea mfano wa utitiri wa taasisi za udhibiti nchini ambazo wakati mwingine zimekuwa zikiingiliana kimajukumu.

“Unakuta TBS (Shirika la Viwango Tanzania), OSHA (Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa Kazi ), TFDA (Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania), ofisi ya mkemia mkuu, Wakala wa Vipimo, NEMC, Tume ya Ushindani, Ewura, Sumatra na nyingine nyingi  na zimekuwa zikihusika katika kutoza tozo na ada mbalimbali,” amesema Magufuli

Amesema siyo katika upande wa udhibiti tu bali hata katika taasisi zinazoratibu ukuzaji wa biashara na ujasiriamali nchini zipo nyingi huku akibainisha wengi wanaifahamu Sido lakini hana uhakika kama wanafahamu juu ya shughuli zinazofanywa na Shirika la Utafiti waMaendeleo ya Viwanda Tanzania  (Tirdo).

“Kutokana na utitiri wa taasisi hizo zimekuwa hazihudumiwi na zimekuwa zinashindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo,” amesema Magufuli