Magufuli atengua, ateua waziri mpya na bosi wa TRA

Muktasari:

  • Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imeelezea mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri ambapo Rais Magufuli ametengua na kuteua waziri mpya pamoja na kumbadili Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amemteua Innocent Bashungwa, kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, akichukua nafasi ya Joseph Kakunda ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi nJUni 8, 2019 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa amesema Rais Magufuli amemteua Edwin Mhede kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), akichukua nafasi ya Charles Kichere.
Msigwa amesema Rais Magufuli amemteua aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe akichukua nafasi ya Erick Shitindi ambaye amestaafu.
Aidha kabla uteuzi waziri mpya wa viwanda na Biashara Innocent Bashungwa alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo.
Kamishna Mkuu mpya wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Edwin Mhede kabla ya uteuzi huu, alikuwa Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara.
Ikulu imeeleza uteuzi wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara utafanywa baadae.