Magufuli atoa onyo kwa madereva Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza jambo na mwanafunzi wa Shule ya Sekondary Karagwe ambaye alikuwa akisafiri na daladala hiyo. PICHA NA IKULU

 


Muktasari:

Taarifa iliyotolewa leo Jumatano na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imesema Rais wa Tanzania, John Magufuli aliyeko Karagwe mkoani Kagera kwa mapumziko amezungumza na abiria na kutoa onyo kwa madereva kuzingatia usalama barabarani


Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amewataka madereva wanaoendesha vyombo vya usafiri wa abiria kuzingatia sheria na taratibu za usalama wa barabarani wakati wote wa safari zao.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Julai 10, 2019 na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imesema Rais Magufuli ameyasema hayo Kijijii cha Kihanga, Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera alipokutana na abiria na dereva wa basi dogo linalofanya safari zake kati ya kati ya Bukoba na Karagwe.

Rais Magufuli amesema ajali nyingi za barabarani husababishwa na ukiukwaji wa sheria na taratibu za usalama barabarani na kwamba jukumu la kuhakikisha sheria na taratibu hizo zinatekelezwa upo kwa watumiaji wote wa barabara hasa madereva wanaoendesha vyombo vya usafiri.

“Poleni na safari ndugu zangu, nimefurahi kuwaona na kuwasalimu, na wewe dereva hongera kwa kazi, fanya kazi zako kwa kuzingatia sheria na taratibu za usalama barabarani, pia kumbuka kusali kabla na baada ya safari” amesema Rais Magufuli

Pia, Rais Magufuli ametumia fursa hiyo kuwaeleza abiria ambao ni wanafunzi kusoma kwa juhudi masomo yao.