Magufuli atoa siri ya kumteua meneja wa darasa la saba

Muktasari:

Rais John Magufuli katika utawala uliopita wa awamu ya nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete akiwa waziri wa ujenzi na uchukuzi aliwahi kumteua mtu mwenye elimu ya darasa la saba kushika wadhifa wa Meneja wa Tamesa mkoa wa Kagera kutokana na kuwa na uwezo kuliko wenye elimu ya shahada.


Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufulia amesema wakati akiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi aliwahi kumuweka Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Tamesa) Mkoa wa Kagera aliye na elimu ya darasa la saba.

Hayo ameyasema leo Alhamisi Juni 13, 2019 katika mkutano uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo alikutana na wabunifu wa kufua umeme kwa kutumia mitambo midogo Jairos Ngailo na John Mwafute ambao ni wakazi wa vijiji vya Msete na Lugenge mkoa wa Njombe 

Magufuli amesema sababu kubwa ya kumuweka darasa la saba ni kutokana na ukusanyaji wake mzuri wa kodi kuliko wenye shahada.

“Nielezee mipango yako vizuri ili nisije kumteua mmoja akawa meneja uzalishaji Tanzania na mwingine  akawa meneja usambazaji wa Tanesco,” amesema

Awali, akizungumza katika mkutano huo, Mwafute amesema licha ya kuwa na elimu ya darasa la saba lakini aliweza kufanikiwa kutengeneza mtambo mdogo wa kufua umeme kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

“Kutokana na nia niliyokuwa nayo niliweza kusaidiwa na wahandisi wa Kijerumani ili kutimiza azma hii na hadi hivi sasa nilipofikia,” amesema Mwafute ambaye anazalisha umeme KV 28

Naye Ngailo anayezalisha umeme KV 15amesema kutokana na shida na gharama aliyokuwa akiipata katika uendeshaji wa biashara zake aliamua kutafuta namna ya kurahisisha suala hilo.

“Nilikuwa nauza pombe za machicha na nilikuwa napata wakati mgumu kuchaji betri katika kijiji kingine na baadaye niliamua kununua jenereta ili niweze kutumia.”

“Lakini mafuta pia yakawa gharama jambo ambalo lilinifanya kutafuta namna ya kuwasha jenereta bila mafuta ndiyo chanzo cha mradi huo,” amesema Ngailo