Magufuli atuma salamu za rambirambi ajali Songwe, aagiza uchunguzi

Muktasari:

  • Rais John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza jamaa zao katika ajali iliyotokea Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe na kusababisha vifo vya watu 19

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza jamaa zao katika ajali iliyotokea Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe na kusababisha vifo vya watu 19.

Ajali hiyo imetokea jana usiku Februari 21, 2019 katika mteremko wa mlima Senjele baada ya lori  lililokuwa likitokea Tunduma kuelekea Mbeya mjini kuligonga  basi la abiria kwa nyuma.

Basi hilo baada ya kugongwa liliminywa katikati baada ya kuligonga lori jingine  lililokuwa mbele yake.

Watu 18 katika basi hilo wote wamefariki dunia pamoja na  dereva wa lori lililogonga basi la abiria.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Februari 22, 2019 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa inaeleza kuwa Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Jenerali mstaafu Nicodemas Mwangela kufikisha salamu zake za pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo vya watu hao.

Rais Magufuli amezitaka mamlaka zinazohusika na usalama wa barabarani mkoani Songwe kufanya uchunguzi wa ajali hiyo na kuchukua hatua zinazostahili pamoja na kujipanga vizuri kukabiliana na matukio ya ajali za barabarani.

Wakati huo huo, Rais Magufuli ametoa mkono wa pole kwa familia ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla ambaye amefiwa na mwanae, Zul jana jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli na mkewe, Janeth  wamefika nyumbani kwa waziri huyo Mikocheni na kukutana na baadhi ya wanafamilia wakiongozwa na mkewe, Dk Bayoum Kigwangalla.

Zul atazikwa leo wilayani Nzega mkoani Tabora.