Magufuli auita mradi wa NSSF ni bomu, atoa maagizo

Muktasari:

Rais wa Tanzania John Magufuli amewataka Watanzania kutoa maoni yao juu ya namna gani nyumba za mradi wa NSSF Kigamboni usioendelezwa zitumike kwa sababu Serikali haiwezi kuendelea kuuangalia bila kuutumia

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema Mradi wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) uliopo Dege Beach Kigamboni jijini Dar es Salaam ni bomu kwa sababu umekaa kwa muda mrefu bila kuendelezwa.

Magufuli amesema hayo leo Jumanne Juni 25, 2019 wakati akifungua ghala na mitambo ya kuhifadhia gesi ya kampuni ya Taifa gesi iliyogharimu Sh150 bilioni kujengwa katika eneo la Kigambaoni jijini Dar es Salaam.

Mradi wa ujenzi wa nyumba hizo zaidi ya 7,000 unajengwa kwa ubia kati NSSF na kampuni ya Azimio Housing Estate Limited.

Magufuli amesema mradi huo ni miongoni mwa changamoto za halmashauri hiyo mpya ya Kigamboni huku akibainisha kuwa siku akiyatembelea atakuwa ameyafanyia kazi.

“Ni mradi bomu, umekaa pale wala hauendelezwi, nimeshaongea na NSSF washughulikie watoe mawazo yao na ninyi wananchi wa Kigamboni mkae mtoe mawazo yenu ni kwa jinsi gani majengo haya tunaweza kuyatumia katika njia iliyo sahihi.”

“Kama ni kuyatoa yawe mabweni ya chuo, nyumba za wafanyakazi au iwe nini, tusubiri huo uchambuzi utakaofanywa katika sehemu zote mbili kwa sababu Serikali ni moja hatuwezi kuacha uwekezaji mkubwa kama huo umekaa bila kazi na hatutoi majibu,” amesema Magufuli

Ameongeza, “Na mimi nina uhakika watendaji ndani ya Serikali hasa wizara inayoshughulikia sera itatusaidia katika kutoa majibu ili kusudi tujue kama unaendelea au hauendelei kama utachukuliwa na Serikali ili kufanya kitu cha maana utakao tusaidia tujue.”

Novemba 13 mwaka 2018, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitembelea mradi huo ambapo alisikitishwa na uharibifu wa mali na wizi unaendelea kwenye eneo la mradi.

Majaliwa aliwaagiza viongozi wa NSSF na Mkurugenzi wa Mkuu kampuni ya Azimio Housing Estate Limited, Mohammed Iqbal  wakutane na Kamishna Mkuu wa  Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili wajadiliane namna ya kudhibiti wizi na kuimarisha ulinzi. 

“Kuna mpango gani wa ulinzi wa mali hapa, mali zinaendelea kuibiwa, tutakuja kuanza ujenzi hapa na kukuta hakuna mali hata moja. Ulinzi lazima uimarishwe pande zote mbili za mradi huu eneo la ujenzi na eneo la kuhifadhia vifaa vya ujenzi,” alisema Majaliwa alipotembelea mradi huo

Mkataba kati ya NSSF na Azimio Housing Estate Limited (AHEL) ulisainiwa mwaka 2012 na kuanzisha kampuni ya hodhi ya “Hifadhi Builders” ambapo AHEL ilikuwa na asilimia 55 na NSSF asilimia 45.

Katika asilimia 55 za AHEL, asilimia 20 ni ardhi iliyotoa kwenye mradi na asilimia 35 angetakiwa kuweka fedha taslimu.

Mradi ulihusisha ujenzi wa nyumba 7,460 ambapo jumla ya gharama za mradi zilikadiriwa kuwa dola za Marekani 653,436,675 ambazo kati yake ujenzi ungegharimu dola 544,530,562 wakati gharama za ardhi zingekuwa dola 108,906,113. Kwa fedha za Tanzania mradi pamoja na ardhi ungegharimu Sh1.5 trilioni.

Hadi kufikia Juni, 2018 NSSF walishailipa kampuni ya Hifadhi Builders Dola 133,838,662.2 kama mchango wake kwenye ujenzi wa mradi huo ambazo ni sawa na sh. bilioni 305.8 wakati kampuni ya Azimio ikitoa Dola 5,500,000 sawa na Sh12.6 bilioni tu.