Magufuli awaanika wanaosingizia ‘ni maagizo kutoka juu’

Wednesday January 2 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Rais John Magufuli juzi usiku alitoa salamu za mwaka mpya wa 2019 kwa kuhoji tabia ya watumishi wa umma kutojiamini katika utendaji wao wa kazi kiasi cha kila jambo wanalolifanya kudai kuwa “ni maagizo kutoka juu”, akisema neno hilo sasa limekuwa kama ugonjwa.

Kauli hiyo ya Rais imekuja kipindi ambacho watendaji mbalimbali serikalini wamekuwa wakitumia neno hilo katika utekelezaji wa majukumu yao, hasa masuala yanayowahusu wananchi.

Akizungumza dakika chache kabla ya kufika saa 6:00 usiku juzi, Rais Magufuli alisema, “Na mara nyingi maagizo yanakuwa hayapo, bali ni utekelezaji wa wajibu wa sheria, wajiamini na wasiwaonee watu lakini watimize wajibu wao.”

Mbali na kuwataka watendaji serikalini kujiamini, Rais Magufuli alisema mwaka huu utakuwa wa mafanikio zaidi kiuchumi na kuwataka Watanzania kudumisha amani, upendo, umoja na mshikamano.

“Ujumbe wangu kwa watumishi wa umma, ni kama nilivyotoa ujumbe kwa Watanzania wengine, wachape kazi, wajiamini,” alisema Rais Magufuli na kuongeza:

“Waachane na utamaduni wa kila kitu wanachokifanya kudai ni maagizo kutoka juu, huo ni ugonjwa ambao umeanza kuwapata watumishi wa umma ambapo kila wanalolifanya hata kama ni kwa mujibu wa sheria hawataki kujiamini, na wanasema hili ni maagizo kutoka juu.”

Advertisement

Akizungumzia mwaka 2018, Rais Magufuli alisema ulikuwa wa mafanikio na mambo mengi yalifanyika katika uchumi wa nchi ambayo Watanzania wameyashuhudia katika maeneo yao na mengine.

“Tuipende Tanzania yetu, amani yetu na umoja wetu na tuendelee kumtanguliza Mungu kila mmoja katika imani yake. Nina imani uchumi kwa mwaka 2019 utapanda zaidi, tulinde amani tuitangulize Tanzania kwanza na kuchapa kazi.”

Aliwataka watumishi wa umma, viongozi, wakulima, wafanyabiashara, wavuvi na wafugaji kuongeza juhudi za uzalishaji mali wakipiga vita rushwa, wizi, ufisadi, ubadhirifu.

Wasomi wazungumzia kauli

Alipotakiwa kutoa maoni yake juu ya kauli ya Rais kuhusu watumishi wa umma kudai kwamba wanatekeleza maagizo kutoka juu kwa hatua wanazochukua, Profesa Samweli Wangwe alisema mtumishi yeyote anapaswa kujiamini na wakati mwingine anapopata maagizo yanayokinzana na sheria wanatakiwa kujishauri na kurudi kuangalia sheria.

“Hata kama ni maagizo wamepewa si kila jambo ni maelekezo, watumishi wanapaswa kufanya vitu kwa kujiamini na kwa kuangalia misingi ya sheria,” alisema.

Mwingine aliyetakiwa kutoa maoni yake ni wakili wa kujitegemea, Dk Onesmo Kyauke ambaye ni alisema inawezekana watumishi wanaotoa kauli hiyo hawajiamini au wanataka kuepuka lawama.

“Mtu kusema ni maelekezo kutoka juu inaondoa ufanisi kwenye kazi kwa kuwa kila kitakachofanyika hakitaonyesha ni wewe umefanya, bali ni maelekezo,” alisema kila mtu anapaswa kufanya kazi kwa utashi na kufuata sheria.

Advertisement