Magufuli awashukia vigogo wa Nishati, Tanesco

Thursday June 13 2019

 

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewashukia viongozi wa Wizara ya Nishati na Tanesco kwa kushindwa kuwasaidia wabunifu wa kufua umeme kutoka Njombe, Jairos Ngailo na John Mwafute maarufu kama Pwagu.

Akizungumza leo Alhamisi ya Juni 13, 2019 katika mkutano na wabunifu hao wa mitambo midogo ya kufua umeme uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Magufuli amesema licha ya wataalamu hao kufanya kazi hiyo kwa muda mrefu, hakuna yeyote aliyejitokeza kuwasaidia.

“Wangekuwa wameshasaidiwa wasingefika hapa. Transfoma zingekuwepo, mkurugenzi wa Tanesco kwao ni Njombe na nina uhakika anaendaga likizo hajafanya lolote, meneja wa Tanesco mkoa (Njombe) nimemsikia akizungumza kuwa hawa waje wanione waende Ewura yeye hakutaka shida.

“Hata wangezalisha umeme ukaleta madhara shida isingekuwa kwa watendaji wa Tanesco, kwa hiyo Mkurugenzi (DED) wa Njombe naye hajaleta taarifa yoyote kuhusiana na wagunduzi hawa tangu mwaka 1980.”

Baada ya maelezo ya Rais Magufuli, Mkurugenzi wa Tanesco, Dk Titus Mwinuka alisema Shirika hilo litatoa Sh30 milioni kwa kila mbunifu.

Pamoja na Tanesco, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk Amos Nungu alichangia Sh10 milioni kwa kila mzalishaji ili kuendeleza miradi hiyo.

Advertisement

Dk Mwinuka amesema licha ya kuwapatia fedha hizo pia watatembelea katika eneo la uzalishaji kwa ajili ya kupima ubora wa umeme na namna ya kuongeza uzalishaji.

“Fedha hizo kila mmoja atapata Sh15 milioni na endapo tutaona umeme una mapungufu katika ziara yetu tutawashauri namna ya kufanya maboresho na tutahakikisha nyaya na transfoma kama zinahitajika wanazipata kwa wakati.” Amesema Dk Mwinuka

Advertisement