VIDEO: Magufuli azindua nyumba za askari, atoa agizo kwa IGP Sirro

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amezindua nyumba za askari katika eneo la Magogo mkoani Geita na kutoa agizo kwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) nchini humo, Simon Sirro kuhakikisha ujenzi wa nyumba zingine nchini unakamilika kwa wakati.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Jumatatu Julai 15, 2019 amezindua nyumba za makazi ya polisi katika eneo la Magogo mkoani Geita nchini humo.

Nyumba hizo 20 ni sehemu ya nyumba 400 ambazo zinapaswa kujengwa kote nchini kwa ajili ya makazi ya askari ambapo Rais Magufuli alitoa Sh10 bilioni kwa ajili ya kazi hiyo.

Akizindua nyumba hizo zilizopewa jina la Sirro Barracks, Rais Magufuli amemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) nchini humo, Simon Sirro kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kama ilivyokusudiwa ili kupunguza changamoto ya makazi kwa askari.

“Kuanzia leo haya makazi yataitwa Sirro Baracks sasa itakuwa ni aibu kama yatabaki kuwa hivi wakati yamebeba jina la IGP, endelea kuliendeleza, zijengwe nyumba nyingi katika eneo hili ili askari wapate nyumba bora za kuishi,” amesema Rais Magufuli

“Hili eneo lilikuwa baya kwa mkoa wa Geita kutokana na utekaji lakini askari wamefanya kazi kubwa sana kuhakikisha eneo hili kwa sasa lipo salama. Askari tembeeni kifua mbele watanzania wanawapenda na wanathamini kazi mnayofanya,”

Magufuli amesema palipo na amani kila kitu kinapatikana hivyo ni jukumu la vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kuwepo.