VIDEO: Magufuli kuipigia debe DRC kujiunga jumuiya ya Afrika Mashariki

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Watu wa kongo (DRC) Mhe. Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo akitambulishwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaack Kamwelwe   kwa viongozi wa kampuni ya upakuaji Makontena ya Tanzania International Containers Terminal Services (TICTS)  alipotembelea Bandari ya Dar es salaam jijini Dar es salaam leo. Picha na Ikulu


Muktasari:

Wakati ombi la DRC kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki (DRC) likiwa limetua kwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Rais wa Rwanda, Paul Kagame, Rais wa Tanzania, John Magufuli ameahidi kuipigia debe nchi hiyo kujiunga na jumuiya hiyo.


Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemueleza Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia na Congo (DRC), Felix Tshisekedi kuwa atampigia debe ili nchi hiyo ijiunge na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Kiongozi mkuu huyo wan chi ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Juni 14, 2019 katika mkutano wa waandishi wa habari akiwa pamoja na Tshisekedi jijini Dar es Salaam.

“Rais Tshisekedi ameniomba nimsaidie kumpigia debe ili nchi yake ikubaliwe kujiunga katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, nami nimeridhia,” amesema Magufuli.

Magufuli amesema wananchi wa DRC na Tanzania ni ndugu na wanashirikiana katika masuala mengi.

Hivi karibuni Congo ilimuandikia barua mwenyekiti wa EAC,  Rais wa Rwanda Paul Kagame kuomba kujiunga na jumuiya hiyo ili kuongeza fursa za kiuchumi na maendeleo.

Leo, Tshisekedi amesema lengo la ziara yake Tanzania ni kukuza mahusiano baina ya nchi hizo mbili na kuongeza wigo wa uchumi na biashara.

Tshisekedi amesema kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili ni kidogo huku kukiwa na idadi ndogo ya wafanyabiasahra waliowekeza kwenye sekta ya madini DRC.

Magufuli amesisitiza  kuhusu kiwango cha biashara baina ya nchi hizo mbili na kutaka ziara ya rais huyo wa DRC kufungua milango ya wafanyabiashara kutoka nchi hiyo kuleta bidhaa na pia kuja kuwekeza nchini katika sekta ya madini, kilimo na viwanda.