Magufuli kuzindua maonyesho ya wafanyabiashara wa nchi 15 za SADC

Ukumbi wa kituo cha kimataifa cha mikutano Mwalimu Nyerere  jijini Dar esSalaam ukiwa umepambwa kwa Bendera 16 za nchi wananchama wa SADC ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa Maonyesho ya nne ya bidhaa za SADC unaotarajiwa kufunguliwa mudi si mrefu  na Rais John Magufuli. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

  • Tayari wafanyabiashara 938 hadi jana Jumapili Agosti 4, 2019 walikuwa wameshasajiliwa kwa ajili ya kushiriki maonyesho ya bidhaa zao katika mabanda yaliyoandaliwa viwanja vya JNICC, Karimjee na Gymkana kuanzia leo hadi Alhamisi.

Dar es salaam. Wafanyabiashara wanaotoka nchi 15 za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika( SADC) wameanza kujitokeza katika Kituo cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere(JNICC), Dar es Salaam nchini Tanzania.

Wafanyabiashara hao wamewasili katika kituo hicho kwa ajili ya kushiriki tukio la uzinduzi wa maonyesho ya bidhaa katika Wiki ya viwanda kwa nchi 16 wanachama wa SADC uzinduzi unaofanywa na Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Nje ya Jengo hilo kuna makundi mbalimbali ya muziki wa asili, yanayotoa burudani kwa ladha zenye tamaduni mbalimbali za Kitanzania.

Tayari wafanyabiashara 938 hadi jana Jumapili Agosti 4, 2019 walikuwa wameshasajiliwa kwa ajili ya kushiriki maonyesho ya bidhaa zao katika mabanda yaliyoandaliwa viwanja vya JNICC, Karimjee na Gymkana kuanzia leo Jumatatu Agosti 5 hadi 8, 2019.

Rais Magufuli tayari amekwisha kuwasili katika viwanja vya JNICC kuzindua maonyesho yanayokutanisha jumla ya wafanyabiashara 2,026 waliosajiliwa kutoka Tanzania na nchi nyingine za Jumuiya hiyo.

Baada ya kuwasili, Rais Magufuli ametembelea mabanda  ya maonyesho ya wafanyabiashara hao.

Ulinzi umeimarishwa katika Jengo hilo lenye kumbi ndogo 16 pamoja na Ukumbi mkubwa wa Selous unaohudumia watu 1,003.

Kuanzia saa 2:00 asubuhi, idadi ya magari na watu wanaoingia ndani ya Jengo hilo ni wengi.

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachoendelea