VIDEO: Maombi ya upinzani yatupwa, Mahakama yaitaka Serikali ijibu hoja

Muktasari:

  • Kesi ndogo ya kutaka kusikilizwa kwa dharura maombi ya upande mmoja wa upinzani kutaka kusitishwa baadhi ya vifungu vya sheria ya vyama vya siasa yaanza kuunguruma Arusha, ikiwakutanisha vigogo wote wa upinzani nchini Tanzania.


Arusha. Mahakama ya Afrika Mashariki, imetupilia mbali maombi ya dharura ya  viongozi wa vyama vya upinzani nchini Tanzania, wakiongozwa na Freeman Mbowe kutaka mahakama hiyo, kuwasikiliza upande mmoja kusitisha utekelezaji wa baadhi ya vifungu katika  sheria ya vyama vya siasa, ambavyo vinadaiwa kukiuka mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo.

Uamuzi huo, umetolewa leo Jumatano Juni 19, 2019 na majaji watano wa mahakama hiyo, katika shauri dogo lililowasilishwa kwa dharura la kuipinga sheria ya vyama vya siasa, ambapo upinzani ulitaka kusikilizwa upande mmoja  kutokana na Serikali  kuanza  uandikishaji wa wapigakura katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

Akisoma uamuzi mdogo katika kesi hiyo, baada ya mahakama hiyo kusitishwa kwa muda, Kiongozi wa jopo la majaji wa Afrika Mashariki katika shauri hilo, Jaji Monica Mugenyi kutoka Uganda amesema kutokana na unyeti wa shauri hilo ni muhimu upande wa Serikali kushirikishwa kujibu hoja.

Jaji Mugenyi amesema hoja za kupinga vifungu vya sheria hiyo ya vyama vya siasa, zinapaswa kufikishwa haraka iwezekanavyo upande wa Serikali ili zijibiwe na baadaye mahakama hiyo itatoa uamuzi.

Majaji wengine waliokuwa wanasikiliza shauri hilo dogo ni Jaji Dk Faustine  Ntezilyayo kutoka Rwanda, Jaji  Dk Charles Nyawelo kutoka Sudani Kusini, Jaji  Charles Nyachai wa Kenya na Jaji Fakihi Jundu wa Tanzania.

Shauri hilo dogo linatarajiwa kuendelea kusikilizwa kabla ya Juni 23, 2019 baada ya Serikali kupewa notisi ya shauri hilo na kujibu hoja za upinzani.

 

Hata hivyo, bado shauri la msingi namba 3/2019 kutaka mahakama ya Afrika ya Mashariki kutengua baadhi ya vifungu katika sheria ya vyama vya siasa linatarajiwa kuendelea katika mahakama hiyo.

Wakizungumza baada ya uamuzi huo, kiongozi wa upinzani bungeni Freeman Mbowe na Kiongozi wa ACT- Wazalendo Zitto Kabwe wamesema wataendelea kupinga sheria hiyo kwani inakiuka katiba na Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema amesema wataingia mitaani kutoa elimu ya wapigakura kwani ni haki ya kikatiba ya watu na hawatasubiri kupata kibali cha msajili wa vyama vya siasa.