Mahakama ya Tanzania yaweka mhuri wa mwisho Bageni anyongwe hadi kufa

Muktasari:

Aliyekuwa Mkuu Upelelezi wa Wilaya ya Kinondoni (OC-CID), Mrakibu wa Polisi (SP) Christopher Bageni aliyehukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa, amegonga ukuta katika jitihada zake za kuepuka adhabu hiyo baada ya kushindwa katika maombi yake ya marejeo ya kuomba mahakama hiyo imfutie hatia na adhabu hiyo.

Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani imetupilia mbali maombi ya marejeo ya aliyekuwa Mkuu Upelelezi wa Wilaya ya Kinondoni (OC-CID), Dar es Salaam nchini Tanzania, Mrakibu wa Polisi (SP) Christopher Bageni aliyehukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa, ambaye alikuwa akiomba Mahakama hiyo ibadilishe uamuzi wake.

Uamuzi wa kutupilia mbali maombi hayo ya Bageni ulioandaliwa na jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo waliosikiliza maombi hayo, umetolewa leo Jumatano, Agosti 14, 2019 na Naibu Msajili Mwandamizi wa  Mahakama ya Rufani, Elizabeth Mkwizu.

Jopo la majaji hao waliosikiliza na kutoa uamuzi wa maombi hayo namba 63 ya mwaka 2016 ni Stella Mugasha (kiongozi), Ferdinarnd Wambali na Rehema Kerefu.

Kwa uamuzi huo ambao ndio wa mwisho, sasa Bageni hana namna nyingine ya kufanya kwani hakuna ngazi nyingine ya mahakama nchini wala hatua nyingine ambayo anaweza kuichukua kuupinga.

Badala yake sasa atasubiri tu utekelezaji wake huku akiombea neema ya rais wa awamu ya sasa au awamu zijazo kumsamehe ama kumwachia huru au kumbadilishia adhabu pengine kuwa ya kifungo kwa mamlaka yake kikatiba kama ataguswa au kuona kuna sababu ya kufanya hivyo.

 

Ofisa huyo wa zamani wa Polisi alihukumiwa na mahakama hiyo adhabu hiyo Septemba 11, 2016, baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge, Morogoro na dereva teksi wa Manzese Dar es Salaam.

Alitiwa hatiani na mahakama hiyo kufuatia rufaa aliyoikata Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), akipinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyomwachia huru yeye na maofisa wenzake wengine wa polisi katika kesi ya msingi.

Lakini siku chache baadaye, alifungua maombi hayo akiiomba mahakama hiyo ifanye marejeo ya hukumu yake hiyo kisha imuondolee hatia na kumfutia adhabu hiyo na iamuru aachiwe huru, akidai kuwa hiyo iliyomtia hatia ina kasoro za dhahiri.

Siku ya usikilizwaji wa maombi hayo, wakili wake Gaudiosus Ishengoma alidai mahakama hiyo ilimtia hatiani bila kumpa fursa ya kumsikiliza kwani ilimtia hatiani kwa ushahidi ambao haupo kwenye kumbukumbu za mahakama na wala haukujadiliwa kwenye rufaa ya DPP.

Hata hivyo, Mahakama hiyo katika uamuzi wake wa leo Jumatano, imetupilia mbali sababu hizo ikisema kwamba hazina msingi kwa kuwa hoja zake hazina msingi kwa kuwa hakuna jambo jipya ambalo Mahakama ililiibua na kwamba hakunyimwa haki ya kusikilizwa kwa kuwa alikuwa na wakili wakati wa rufaa hiyo.

Mkwizu alisema kuwa Mahakama hiyo ilitekeleza majukumu yake na kwamba katika kumtia hatiani ilifanya tu uchambuzi wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani ukiwemo wa aliyekuwa mshtakiwa mwenza, aliyeeleza ukweli wa tukio na Bageni hakuupinga.

“Mwombaji ameshindwa kuonesha makosa kwenye hukumu hii (iliyomtia hatiani), kama alivyodai kwenye sababu zake za maombi. Kwa hiyo hatuna namna nyingine zaidi ya kuyatupilia mbali maombi haya, kwani.”, alisema Mkwizu.

Katika kesi ya msingi, Bageni na wenzake 13, walikuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya wafanyabiashara hao Sabinus Chigumbi (Jongo) na ndugu yake Ephrahim Chigumbi na mwenzao Mathias Lunkombe pamoja na Juma Ndugu, dereva teksi aliyekuwa akiwaendesha,

Walikuwa wakidaiwa kuwaua kwa kupigwa risasi katika msitu wa Pande wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Januari 14, 2008.

Kabla ya kuuawa, walitiwa mbaroni na askari hao eneo la Sinza Palestina nyumbani kwa mchimbaji mwenzao, ambao waliwafunga pingu wakiwatuhumu kuhisika katika uporaji wa pesa za kampuni ya Bidco na baadaye polisi walidai kuwa walifariki wakati wakirushiana nao risasi.

Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa Agosti 17, 2009 na aliyekuwa Jaji Kiongozi Salum Massati, aliyeisikiliza, ingawa alikiri kuwa kwa mujibu ushahidi uliowasilishwa mahakamani, Bageni alikuwepo ndiye aliyeongoza msafara wa washtakiwa kwenda eneo la mauaji, lakini iliwaachia huru wote.

Jaji Massati alisema kuwa kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, mauaji hayo yalitekelezwa na Koplo Saad Alawi, ambaye hakuwa miongoni mwa washtakiwa (hadi sasa hajulikani aliko) na kwamba hakuna ushahidi kwamba Bageni aliamuru au alisaidia au aliwezesha mauaji hayo.

Lakini baada ya DPP kukata rufaa, Mahakama ya Rufani katika hukumu iliyotolewa na jopo la majaji watatu Bernard Luanda (kiongozi wa jopo), Sauda Mjasiri na Semistocles Kaijage ilimtia hatiani Bageni na kumhukumu adhabu hiyo.