Mahakama yamsafisha Shakira tuhuma za kuiga wimbo

Muktasari:

Nyota huyo wa muziki wa Colombia ambaye anaishi pamoja na beki wa Barcelona, Gerard Pique katika jiji hilo, alituhumiwa kukopi sauti na mashairin ya wimbo wa mwanamuziki mwingine ambaye wanadai hawamjui.

 


Madrid, Hispania/AFP. Mahakama ya Hispania imemsafisha wanamuziki nyota wa Colombia, Shakira na Carlos Vives dhidi ya mashtaka kuwa waliiga sehemu ya mashairi katima wimbo wao wa "La Bicicleta" ulioshinda tuzo ya Grammy.

Livan Rafael Castellanos, mwimbaji wa Cuban anayejulikana zaidi kwa jina la Livam, alidai kuwa wimbo huo ulikopi sehemu ya sauti na mashairi ya wimbo wake wa "Yo te quiero tanto (I love you so much)".

"Hakuna uigaji wowote kama inavyodaiwa na mdai katika mashtaka yake," mahakama hiyo ya biashara ilisema katika uamuzi wake.

kampuni ya kurekodi muziki ya MDRB ilifungua kesi hiyo mwaka 2017 jijini Madrid kwa niaba ya Livam.

Mwezi Machi, Shakira, 42, ambaye anaishi Barcelona, aliiambia mahakama kuwa "hakuwahi kusikia" wimbo wa Livam kabla ya kutunga kibao hicho.

Vives, 57, pia alisema haujui wimbo huo wala hamjui Livam.

Wimbo wa "La Bicicleta (baiskeli)" ulishinda tuzo mbili kati ya tatu katika tamasha kubwa la Tuzo za Grammy Latino mkwaka mwaka 2016. Tuzo hizo ni Wimbo wa Mwaka na Rekodi ya Mwaka.

Katika wimbo huo, Shakira na Vives wanaimba "que te sueno y que te quiero tanto (nakuota na nakupenda sana)"), wakati Livam anasema "yo te quiero, yo te quiero tanto (nakupenda, nakupenda sana)".

Lakini mahakama ilisema maneno hayo ni ya kawaida na hutumiwa katika nyimbo na mashairi ya aina zote wakati wote katika historia.

Kesi nyingine

Shakira, ambaye anaishi na beki wa klabu ya FC Barcelona, Gerard Pique na watoto wao wawili wa kiume, anatarajiwa kupanda mahakamani tena mwezi ujao kwa tuhuma za kukwepa kodi ya dola 16.3 milioni za Kimarekani, shtaka ambalo mwanasheria wake analikana.

Anatuhumiwa kutolipa kodi nchini Hispania licha ya kuishi huko kati ya mwaka 2011 na 2014, kwa mujibu wa waendesha mashtaka.